May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tedros mgombea pekee, kuendelea kuongoza WHO

Spread the love

MKUU wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus ana uhakika wa kuiongoza taasisi hiyo kwa muhula wa pili baada ya kupigiwa kura inayomfanya kuwa mtu pekee atakayegombea uchaguzi wa wadhifa huo mwezi Mei mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Tedros ambaye ni kiongozi wa kwanza Mwafrika wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, ameshukuru kwa uungwaji mkono alioupata, baada ya bodi ya utendaji ya WHO kupiga kura ya siri iliyoidhinisha uteuzi wake wa kuwa mgombea pekee kwa wadhifa huo.

Tedros ni mmoja wa viongozi waliogonga vichwa vya habari katika mapambano ya kimataifa ya janga la COVID-19, alikiri kuwa muhula wake wa kwanza wa miaka mitano ulikuwa na changamoto na mgumu na akasema ni heshima kubwa kupewa fursa ya kuendelea kupambana.

Waziri huyo wa zamani wa Afya na mambo ya nje wa Ethiopia, anatarajiwa kuchaguliwa bila kipingamizi wakati mataifa yote 194 – wanachama wa WHO yatapiga kura zao kumchagua Mkurugenzi Mkuu mwezi Mei.

Tangu kuanza kwa janga la COVID 19 duniani miaka miwili iliyopita, Tedros aliye na miaka 56 na mtaalamu wa ugonjwa wa Malaria, amepokea sifa nyingi kwa namna alivyoiongoza dunia katika mapambano ya janga hilo.

Mataifa ya Afrika yamefurahishwa na umakini unaotolewa kwa bara hilo kutokana na kampeni ya Tedros ya kuyasaidia mataifa masikini kupata chanjo dhidi ya COVID 19.

Hata hivyo, upinzani wa Tedros umekuja kutoka ndani ya taifa lake.

Serikali ya Ethiopia imepuuza matamshi yake juu ya hali ya mgogoro wa kibinaadamu katika eneo la Tigray katika vita vilivyodumu miezi 14.

Mwanzoni mwa mwezi huu Tedros aliifananisha hali katika eneo hilo kuwa sawa na jehanamu na kuituhumu serikali ya Ethiopia kuzuia dawa na msaada mwengine kufika katika maeneo yaliyoathirika.

Kutokana na kauli hiyo Ethiopia ilitaka achunguzwe kwa madai ya kuhusika na hatua za kuunga mkono vikosi vya wapiganaji wa Tigray wanaopambana na serikali kuu ya Ethiopia.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa bodi kuu ya utendaji ya WHO, Patrick Amoth amearifu kwamba taasisi hiyo itaahirisha kutoa uamuzi kuhusu ombi lililotolewa.

Amoth amesema ombi la serikali ya Ethiopia ni suala gumu lenye kubeba athari za kisiasa na liko nje ya mfumo wa taratibu za kamati hiyo na kupendekeza suala hilo liwekwe kando na kujadiliwa na wale wanaohusika katika wakati mwafaka.

error: Content is protected !!