September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCU yafuta vyuo vikuu, vishirikishi

Katibu Mtendaji TCU, Charles Kihampa

Spread the love

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefuta hati za usajili za vyuo vitatu na chuo kikuu kishiriki kimoja, baada ya kubaini kukosa uwezo wa kujiendesha. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea).

Vyuo hivyo ni, Chuo Kikuu Kishiriki cha Josia Kibira (JOKUCo), Chuo Kikuu cha Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 21 Januari 2020, Profesa Charles Kihampa, Katibu Mtendaji TCU amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya vyuo hivyo kushindwa kufanya maboresho.

“Licha ya tume kutoa ushauri na mafunzo ya namna mbalimbali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundisha, pamoja na kutoa muda wa kufanya maboresho kwenye maeneo mbalimbali yaliyobainishwa kwa zaidi ya miaka mitatu, hawakufanya kama ilivyotakiwa,” amesema Prof. Kihampa.

Amesema, vyuo hivyo vilikuwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali watu na fedha, na kwamba haviwezi kuondoa changamoto hizo, hata kama vingepewa muda zaidi wa kutatua changamoto hizo.

“Tume katika vikao vyake vya 89,90,91, 92 na 97 vilivyofanyika kati ya mwezi Agosti 2019 na Januari 2020, imefuta hati za usajili za vyuo hivyo,” amesema Pro. Kihampa.

Wakati huo huo, Prof. Kihampa amesema TCU imeridhia maombi ya wamiliki wa vyuo kufuta vyuo vikuu vishiriki viwili na vituo vitatu vya vyuo vikuu.

Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo (AJUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kadinali Rugambwa (CARUMUCo) na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji-Kituo cha Dar es Salaam (TEKU-Dar).

Vyengine ni, Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania- Kituo cha Mt. Marko (SJUT-St. Mark’s Center) na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia Kituo cha Arusha (JKUAT-Arusha Center.).

“Kufuatia mashauriano na maombi yaliyofanywa na wamiliki wa vyuo hivyo kusitisha utoaji wamafunzo, tume katika kjikao chake namba 97 cha Januari 20, 2020 imeridhia maombi ya wamiliki hao ya kusitisha utoaji mafunzo. Hivyo imefuta hati za usajili,” amesema Prof. Kihampa.

Prof. Kihampa amesema hatua hizo zimechukulia baada ya TCU kufanya ukaguzi maalumu wa kitaaluma, kwa taasisi 64 za vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki a vituo vya vyuo vikuu.

“Lengo lilikuwa kuhakikisha elimu ya juu itolewayo inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda na kimataifa. Matokeo ya ukaguzi yalibainisha kasoro mbalimbali katika uendeshaji wa vyuo vikuu nchini,” amesema Prof. Kihampa

Prof. Kihampa amesema katika ukaguzi huo, vyuo 45 vilikutwa na kasoro ndogondogo ambapo vilipewa ushauri na kujirekebisha katika kipindi kifupi, na kuruhusiwa kuendelea na utoaji wa elimu ya juu.

Pia, vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa na kupewa ushauri na muda wa marekebisho, hata hivyo havikuweza kurekebisha katika kipindi kifupi, na kuzuiwa kudahili wanafunzi wapya kuanzia mwaka wa masomo 2017/18.

Hata hivyo, amesema hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka 2019 vyuo vikuu nane kati ya 19 vilivyositishwa udahili, vilifanya marekebisho na kuruhusiwa kudahili na kuendelea kutoa mafunzo kwa baadhi ya program.

error: Content is protected !!