August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCU wafungua dirisha la kwanza la udahili 2022/23

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa

Spread the love

 

DIRISHA la kwanza la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (shahada ya kwanza) kwa mwaka wa masomo wa 2022/2023 limefunguliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) huku ikianisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, ametangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo leo Ijumaa Julai 8, 2022 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini, ambapo amesema hatua hiyo inakuja baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita.

Prof. Kihampa amesema, dirisha hilo limefunguliwa rasmi kuanzia leo Julai 8, 2022 na litafungwa Agosti 5, 2022.

Amesema, udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita; wenye Stashahada (Ordinary Diploma) na waliomaliza programu ya ‘Foundation’ ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Prof. Kihampa amesema ili waombaji wafahamu sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu wanatakiwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU huku pia wakitakiwa kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua na kwamba maelekezo ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo vikuu husika.

Pia Prof. Kihampa amewapa tahadhari waombaji wote wa shahada ya kwanza ikiwa watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote juu ya udahili kuwasiliana moja kwa moja na vyuo husika ama TCU.

“Kama muombaji atakutana na changamoto yoyote nashauri apate maelezo sahihi kutoka katika chuo chake au TCU na siyo kusikia taarifa nyingine kutoka kwa watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini,” amesema Prof. Kihampa.

Amesema masuala muhimu ambayo waombaji wanapaswa kuzingatia ni pamoja na kusoma muongozo wa udahili na kuuelewa, kuingia kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektoniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa huku pia waombaji wenye vyeti vinavyoyolewa na NECTA au NACTE wakitakiwa kupata idhibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Pia Prof. Kihampa amewaomba wanachuo na wananchi kwa ujumla kuhudhuria Maonyesho ya 17 ya Vyuo vya Elimu ya Juu na Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 18 hadi Julai 23, 2022.

error: Content is protected !!