January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yawatwisha mzigo viongozi wa dini

Spread the love

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma amewataka viongozi wa dini kutoa elimu vya kutosha kwa waumini wao inayohusu ubaya wa matumizi yasiyotija ya mitandao ya mawasiliano.

Nkoma amesema jijini Dar es Salaam leo kwamba kutokana na watu wengi kumudu kumiliki simu za kisasa, imekuwa rahisi kujikita katika kufanya mawasiliano kwenye mitandao kama Facebook, Whatsapp, Instagram na Badoo. Anaripoti Sarafina Lidwino.

Amezungumza hayo leo asubuhi kwenye ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya kutwa kwa viongozi wa dini mbalimbali kuhusiana na athari za matumizi mabaya ya mitandao ya mawasiliano.

Alisema kwamba viongozi wa dini ni sehemu muhimu ya mawasiliono kwa kuwa wanapokutana na waumini wanatoa elimu ya kuhamasisha jinsi ya kuwa wachamungu na kuishi na watu vizuri.

Mkurugenzi wa Tume ya Mawasiliano alisema watumiaji wa mitandao wanapatikana kwa wingi kwenye nyumba za ibada ambako vijana ni asilimia kubwa, na ndio hasa wanaolengwa katika kutambua matumizi mazuri ya mitandao ya mawasiliano.

“Kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi ambalo huwa linafuatilia na kuchukuwa sheria kwa wote wanaotumia mitandao kinyume na sheria, kama vile kutumia lugha ya matusi, kutumiana picha za utupu, ugombanishi na wizi ndivyo ilivyo kwenu Viongozi wa Dini mnasema ni dhambi. Ninaimani nyinyi mkikemea mabaya haya, wananchi wengi watabadilika,” amesema Nkoma.

Jenerali Nkoma alisema kwamba iwapo viongozi wa dini watatimiza wajibu wao kwa kikamilifu na kwa uangalifu mkubwa, waumini wao watapata elimu nzuri na endelevu, elimu ambayo itakuwa inahamasisha wafuate tu yale mema na kuachana na mambo mabaya yakiwemo yanayotokana na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

error: Content is protected !!