MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekusanya Sh. 9.6 bilioni kutoka kwa kampuni za simu za mkononi kutokana na faini walizotakiwa kulipa baada ya kufanya usajili wa laini za simu bila vitambulisho na kutofuata utaratibu, anaandika Irene Emmanuel.
Kampuni zilizopigwa faini na TCRA kutokana na makosa hayo ya kusajili laini za wateja wa simu bila ya kuwa na vitambulisho na kutofuata utaratibu ni pamoja na Vodacom, Tigo, Zantel, Airtel, Smart na Halotel.
Mhandisi James Kilaba, Mkurugenzi wa TCRA, amezitaja kampuni zilizotozwa faini hiyo na kiwango kwenye mabano ni Airtel (Sh1.08 bilioni), Smart (Sh1.3 bilioni), Vodacom (Sh945 milioni), Zantel (Sh105 milioni) na Halotel (Sh1.6 bilioni).
Mkurugenzi huyo amesema hiyo siyo mara ya kwanza kwa kampuni hizo kufanya makosa hayo, na kutolana na kurudia makosa wamepigwa faini nyingine kwa kufanya kosa mara mbili.
Kampuni zilizopigwa faini kutokana na kurudia kosa ni Airtel imetozwa Sh542 milioni, Smart (Sh37 milioni), Tigo (Sh625 milioni), Zantel (Sh52 milioni) na Halotel (Sh822 milioni).
Mhandisi Kilaba amesema kampuni hizo zimetozwa Sh. 500 milioni kila moja kwa kosa la kuathiri na kuhatarisha usalama wa umma na jamii ya Watanzania kwa kusajili laini bila kufuata utaratibu.
Leave a comment