April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yashusha nyundo kwa Global TV, EATV

Spread the love

KITUO cha Runinga cha EATV, Global TV na Le Mutuzi Online, vimepewa onyo na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kukiuka kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2018. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 3 Septemba 2019 jijini Dar es Salaam, Valerie Msoka Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA amesema Tv hizo za mtandaoni zimeamriwa kuomba radhi siku saba mfululizo kuanzia tarehe 4 Septemba 2019.

Akielezea makosa ya vituo hivyo, Msoka amesema zilikiuka kauni za maudhui ya mtandaoni kwa kuonesha miili ya watu waliofariki dunia kwa kuungua moto katika ajali ya lori la mafuta iliyotokea  tarehe 10 Agosti 2019 mkoani Morogoro.

Msoka ameeleza kuwa, Le Mutuz Online Tv na Global Tv zilichelewa kuondoa picha hizo katika chaneli zao, kinyume na matakwa ya kanuni za maudhui ya mtandaoni, zinazotaka wahusika kuondoa picha zinazokiuka maudhui ndani ya saa 12.

“Baadhi ya vyombo hivyo viligundua  makosa yao na kuondoa hizo picha hizo mara moja, ieleweke wazi kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 16 kipengele kidogo cha 1 na 2,  ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroni na Posta, ‘maudhui mtandaoni’ ya mwaka 2018 inampa fursa mtoa maudhui kurekebisha au kuondoa maudhui aliyochapisha ambayo yanakwenda kinyume na kanuni hizo au sheria nyingine za nchi ndani ya saa 12,” amesema Msoka.

Msoka amesema mnamo tarehe 28 Agosti 2019 viongozi wa Tv hizo walihojiwa na Kamati ya Maudhui ya TCRA kwa kushindwa kujirekebisha ndani ya muda uliowekwa na kanuni, ambapo walikiri kufanya kosa na kuomba msamaha.

 “Katika utetezi wake Le Mutuz Online Tv ilieleza kuwa kosa hilo lilisababishwa na uzembe wa msimamizi wao wa maudhui kwa kutozingatia weledi, aidha ilikiri kosa na iliomba isamehewe kwa kosa lililofanyika na kuahidi kutorudia kosa,” amesema Msoka na kuongeza.

“Katika utetezi wake Global Tv ilisema ilichukua tahadhari kubwa kuziba picha kwa kuwekea kivuli lakini ilitokea tatizo la kiufundi na kivuli hakikuonekana, ilikiri kosa na kuomba radhi na kuahidi kutorudia kosa na kusema imeshaondoa picha.”

Msoka amesema baada ya kamati hiyo kusikiliza utetezi wa Tv hizo, ilijiridhisha kuwa zilikiuka kanuni za maudhui ya mtandaoni na kuzipa onyo pamoja na maelekezo

“Baada ya kuskiliza kwa kina utetezi, kamati ya maudhui imeridhika kuwa zimekiuka kanuni za mawasiliano. Hivyo kamati inashauri kuimarisha usimamaizi makini wa chaneli zao ili kuhakikisha maudhui yao ni salama na hayakiuki maadili kabla ya kuchapisha mitandaoni. Pia zinaaswa kuwajengea uwezo watu wao,” amesema  Msoka.

Katika hatua nyingine, Msoka amesema kamati ya maudhui imeipa onyo kituo cha runinga cha EATV kwa kosa la kurusha maudhui ya watu wazima wakati ambao watoto wanasikia, kupitia kipindi chake cha Dadaz kwenye kipengele cha ‘Mtu Kati’.

“Kwa upande wa EATV tarehe 2 Julai 2019 kupitia kipindi chake cha Dadaz katika kipengele cha mtu kati walirusha maudhui ya watu wazima wakati ambao watoto wanasikia, katika utetezi wao EATV ilisema kipindi ni cha kuelimisha lakini watangazaji walitumia maneno yasiyo faa,” amesema Msoka na kuongeza:

“Kutokana na makosa hayo, baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi, kamati ya maudhui imejiridha imekiuka kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta na Madhui ya Utangazaji ya Mwaka 2018, hivyo basi EATV wanapewa onyo kali, kuhakikisha watumishi wake wote wanazielewa na kuzifuata kanuni za utangazaji ili kuiwezesha kuepuka kuvunja sheria na kanuni.”

error: Content is protected !!