August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yapewa ujumbe wa serikali

Spread the love

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeombwa kuishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalumu utakaokuwa na uwezo wa kujenga minara ya simu katika sehemu mbambali, ili nchi nzima iweze kuenea mitandao ya mawasiliano ya simu, anaandika Jumbe Ismail.

Akifungua semina ya siku moja kuhusu mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa simu za kiganjani Saidi Amanzi, Mkuu wa Wilaya ya Singida amesema kwamba, inafaa zaidi kuwa na mnara mmoja utakaotumiwa na kampuni zote za simu badala ya kila kampuni kuwa na mnara wake.

Kwa mujibu wa Amanzi, kuwepo kwa minara mingi katika maeneo mbalimbali kutasaidia pia nchi nzima kuweza kuenea mitandao ya mawasiliano ya simu.

“Na nimewaomba kwamba, wenzetu sasa wao wameshika mpini basi wasimamie shughuli zote zinazohusu upande huu wa mawasiliano, tumeona mambo mengi yamekuwa yakifanyika ya ovyo ovyo huko, sasa kwa kutumia utaratibu huu nadhani sasa yatakuwa yanatambulika,” amefafanua.

Amesisitiza kuwa, anaamini kwamba kwa utaratibu walioanza kuufanya, hata wale waliokuwa wanakusudia kufanya mambo ya uovu, kwa hivi sasa wataacha.

Amanzi amesema TCRA kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Tume ya Ushindaji (FCC) wasisite kutumia nafasi zao ili kuhakikisha Tanzania haiwi dampo la vitu bandia na badala yake kuwepo bidhaa zenye viwango na ubora unaotakiwa.

Kwa upande wao wafanyabiasha wanaonunua na kuuza simu za viganjani kutoka nje ya nchi wameiomba TCRA kuwatoa hofu iwapo namba za utambulisho walizotoa kwa ajili ya kubaini simu bandia zitaweza kufanyakazi ya kuzitambua simu bandia wanapokuwa nje ya Tanzania huku wakisisitiza kuwa elimu inayotolewa na mamlaka hiyo imechelewa kuwafikia mapema,jambo ambalo linaweza kuchangia kuchelewesha ukuaji wa uchumi wa nchi.

Awali Dk Ally Simba Mkurugenzi mkuu wa TCRA alitumia fursa hiyo kwa kuwataka watanzania kuondokana na dhana potofu kwamba simu za tochi na zile zenye kuuzwa kwa bei ndogo ni bandia na kuamini kuwa simu zenye bei kubwa kama vile smati ndizo simu halali kutumika kuanzia sasa.

Naye Ofisa Uhusiano wa Shirika la Viwango (TBS),Roida Andusamile aliweka wazi kwa watoa huduma na wadau wa sekta ya mawasiliano kwamba tangu mwaka 2012 shirika hilo kwa kushirikiana na mawakala wa kimataifa, limeanzisha utaratibu wa kukagua bidhaa zinazotoka nje ya nchi kabla hazijaja nchini.

Hata hivyo ofisa uhusiano huyo wa TBS alionyesha masikitiko yake kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao siyo waaminifu na wamekuwa wakiingiza bidhaa kupitia njia zisizokuwa halali, kwa madai kuwa bidhaa nyingi hupita katika bandari ya Dar-es-Salaam.

“Sasa kinachosikitisha kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiingiza bidhaa kupitia njia zisizo halali, bidhaa nyingi zinapita katika bandari ya Dar-es-Salaam, lakini wafanyabiashara wasiowaaminifu wametumia mwanya wa kuangalia ambako taasisi kama shirika la viwango au TRA hawapo ndipo wanapopitisha bidhaa hizo”alibainsiaha.

error: Content is protected !!