May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yaipungzia adhabu Wasafi TV, kurejea 28 Februari

Naseeb Abdul 'Diamond Platnum’

Spread the love

 

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeipunguzia adhabu Wasafi TV, kutoka miezi sita hadi mwezi mmoja na siku 22. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

TCRA iliifungia Wasafi TV kufanya kazi kuanzia 6 Januari hadi 6 Julai 2021, kutokana na kukiuka kanuni za maudhui ya utangazaji wa redio na televisheni ya mwaka 2018.

Kilichowaponza ni kurusha matangazo yakimwonesha msanii Gigy Money akicheza jukwaani kwa mitindo ya kuonesha utupu wa mwili wake, kinyume na kanuni za utangazaji.

Tarehe 1 Januari 2021, kuanzia saa 2 hadi saa 5 usiku kupitia kipindi cha ‘Tamasha Tumewasha” walirusha matangazo hayo yaliyomwonesha Gigy Money.

Hata hivyo, leo Alhamisi tarehe 4 Februari 2021, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA ametoa taarifa akisema, baada ya uamuzi huo, 21 Januari 2021, Wasafi TV iliwasilisha maombi TCRA na vielelezo zaidi ikiomba kupitia upya uamuzi wake.

“Tarehe 28 Januari 2021, Wasafi TV ilifika TCRA kwa ajili ya kusikilizwa maombi hayo, Wasafi iliwasilisha ushahidi mpya kuonesha kuwa endapo ushahidi huo ungewasilishwa awali wakati wa usikilizwaji, TCRA isingeweza kutoa adhabu ya kufungiwa miezi sita,” imeeleza taarifa hiyo

“Vilevile, Wasafi TV ilikiri kurusha matangazo mbushara kinyume na masharti ya leseni yao. Wasafi iliiomba TCRA kupitia upya uamuzi wake na kupunguza adhabu yake.”

Baada ya Wasafi TV kusikilizwa, TCRA imeamua “Wasafi TV itaendelea kutumikia adhabu hiyo mpaka tarehe 28 Februari 2021.”

Hii ni tofauti na adhabu ya miezi sita iliyokuwa imetolewa awali kwa Wasafi ambayo Ofisa Mtendaji Mkuu wake ni, Naseeb Abdul maarufu Diamond.

Uamuzi huo mpya wa TCRA, wameufanya ikiwa imepita wiki kadhaa baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kusema, suala hilo litaangaliwa upya ili kulinda uwekezaji.

Tarehe 9 Januari 2021, Waziri Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema, TCRA inasimamia masuala ya udhibiti na yeye (waziri), ni mlezi hivyo, kupitia rufaa waliyokuwa wamekata, ingeangaliwa ili kutoathiri ajira za wafanyakazi.

“Sisi kama wizara, kwenye jukumu la ulezi na kulitizama kwa mapana, inagusa ajira kwa vijana walioajiliwa na TV hii, inagusa uwekezaji, tumewasiliana na TCRA kwa upande wao. Kupitia rufaa yao, hilo jambo litapatiwa mwafaka muda si mrefu,” alisema Waziri Bashungwa.

Ushauri huo kuhusu kulinda ajira kwa kuingilia suala hilo hadi adhabu kupunguzwa, ni tofauti na kile ambacho baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikifungiwa, pasina kupunguziwa adhabu.

Baadhi ya magazeti ambayo yamefungiwa na hayajulikani yatarejea tena lini ni Tanzania Daima, MwanaHALISI, Mseto na Mawio.

error: Content is protected !!