KUELEKEA uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imendesha semina kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini humo ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao ipasavyo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu… (endelea)
Semina hiyo imendeshwa leo Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2020 makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam ikihusisha waandishi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la polisi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema, semina hii imekuwa na manufaa makubwa kwani vyombo vya habari kupitia vipindi vyao viliendesha mahojiano mbalimbali na wagombea kutoka vyama vya siasa na kuwapa fursa Watanzania kusikiliza sera zao.
“Vipindi hivyo viliwapa fursa wananchi katika kuwasikiliza na kuwafahamu wagombea ambao wanataka kuwaongoza sambamba na kutoa elimu ya kuwahamasisha wananchi kwenda kupiga kura kwa manufaa ya nchi” amesema Kilaba
Aidha, Mhandisi Kilaba amesema, waliona sio vyema kufanya shughuli hiyo peke yao, ndipo walipoamua kuchukua hatua ya kuwashirikisha wawakilishi kutoka NEC pamoja na jeshi la polisi.
Kwa upande wa jeshi la polisi ambalo liliwakilishwa na Mayala Towo ambaye ni kaimu kamanda wa polisi kitengo cha Tehama makao makuu amesema, waandishi wanapaswa kuwa makini katika kutekeleza wajibu wao kwenye uchaguzi huu ikiwa sambamba na kuangalia usalama wao.
“Polisi tunayo macho ya kuona lakini kuna nyakati nyingine lazima ujitafakari pia, uhalifu haupo kama tunavyoufikilia sisi, usipende kujichanganya na watu kwa sababu sisi polisi ndio wenye kujua usalama wa mahali husika uko vipi,” amesema Towo
Leave a comment