January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yadhamini simu za dharura polisi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe (mwenye miwani meusi) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Jeshi la Polisi na TCRA

Spread the love

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, amezindua rasmi mradi wa simu za dharura kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Namba hizo ni 111 na 112. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa makao makuu ya kanda hiyo, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Prof. Makeme Mbarawa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Joseph Kilongola na Makamishna Suleiman Kova.

Akiuzungumzia mradi huo, Kilongola kwa niaba ya TCRA amesema, lengo la kuazisha mawasiliano hayo ya dharura lilianza tangu mwaka 2013 ambapo walishirikiana na Jeshi la Polisi hadi kufikia leo.

Amesema, waliamua kufanya hivyo baada ya kutokuwa na kituo cha simu za dharura Polisi kwa muda mrefu kutokana na uharibifu wa miundombinu ambapo mvua iliharibu mitambo ya mawasiliano.

“Baada ya shida hiyo ya muda mrefu, ndipo TCRA ikatoa tena kiasi cha Sh. 50 milioni kwa ajili ya kurudisha mitambo iliyoharibika, kukarabati chumba cha kuweka mitambo hiyo, pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa 65 watakaotoa huduma hizo,” amesema Kilongola.

Naye Kova, amesema, “…tunawashukuru sana TCRA  kwa kudhamini mradi huu, kwani wananchi wamepata tabu kwa muda mrefu jinsi ya kutoa taarifa za uharifu. Tunaimani kuwepo kwa namba hizi kutapunguza uharifu nchini.”

Aidha, Kova amesema, kuna kompyuta 12 za kupokea simu kwa wakati mmoja na zina uwezo wa kurekodi na kuhifadhi taarifa zote za mpigaji simu, pia mitambo ina uwezo wa kupokea simu kutoka mikoa yote.

Kwa upande wake, Chikawe amewasihi wananchi kuitumia fursa hiyo kwa kutoa taarifa muhimu na sio kufanya mizaha.

“Pia nitoe rai kwa maafisa wote mliofundishwa kutumia mitambo hiyo kuwa wasikivu na kuyapokea matatizo ya wananchi. Isije kutokea mtu ana dharura anapiga simu bila kupata msaada, pia msiwe wakali kwa wapigaji simu,” amesema Chikawe

error: Content is protected !!