October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TCRA yabariki ongezeko bei za bando, wasema ni jambo la kawaida

Spread the love

 

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema mabadiliko ya bei za bando iliyofanywa na baadhi ya kampuni za simu za mkononi nchini ni jambo la kawaida katika soko la ushindani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya bei ya bando hizo kupanda ghafla na kuibua malalamiko kwa mara nyingine kwa watumiaji wa huduma hizo nchini.

Mathalani aliyekuwa akinunua bando la Tigo la mwezi kwa Sh. 20,000 alikuwa akipatiwa dakika, sms na GB10 lakini sasa anapata GB 6.5. Aliyekuwa akijiunga bando la Sh. 35,000 kwa mwezi alikuwa akipata GB30 lakini sasa ni GB 25.

Mabadiliko kama hayo yamefanywa pia na kampuni ya Airtel ambapo mtumiaji alikuwa akipata GB 1 na dakika kadhaa kwa siku tatu kwa gharama ya Sh 1,000 lakini sasa ni mteja anapatiwa MB 500 pekee.

Aidha, kutokana na mabadiliko hayo ambayo yametokea pia katika mitandao mingine ya kampuni za simu za mkononi nchini, MwanaHALISI Online imezungumza na Mkurugenzi wa Masuala ya Sekta wa Mamlaka hiyo, Dk. Emmanuel Manasseh kuhusu mabadiliko hayo.

Akizungumzia mabadiliko hayo leo Jumatatu tarehe 4 Oktoba 2021, Mkurugenzi huyo amesema sheria na kanuni hazimzuii mtoa huduma kubadilisha bei za vifurushi hivyo.

Mkurugenzi wa Masuala ya Sekta wa Mamlaka TCRA, Dk. Emmanuel Manasseh

“TCRA kazi yetu ni kusimamia gharama, bei za huduma za mawasiliano lakini sheria na kanuni zetu hazimfungi mtoa huduma kubadilisha bei zake. Soko letu ni la ushindani si la mtu mmoja.”

“Mabadiliko ya bei hayakuanza leo au jana, bei za bando za mwaka 2011 si kama za sasa ambazo zimepungua,” amesema.

Alipoulizwa, kama kuna dokezo limeletwa kabla ya kuipitisha, Dk. Manaseh amesema kampuni hizo za simu zilipeleka na baada ya TCRA kuzipitia waliona ziko sahihi na hawakuona sababu ya kuzizuia.

Dk. Manasseh amesema, mabadiliko ya awali ambayo bei za bando zilipanda kisha zikarejeshwa kama awali, utaratibu wake haukufuatwa.

“Kwa sababu mtoa huduma haruhusiwi kubadili vifurushi vyote, ndivyo ilivyokuwa tofauti na sasa,” amesema.

Ameongeza kuwa katika biashara kubadilisha bei kwenye soko la ushindani ni jambo la kawaida.

“Mtoa huduma anaweza kubadilisha bei akaona haiendani na soko anarudi kwetu kutuambia hii naibadili na sisi tunaona yuko ndani ya utaratibu tunamruhusu,” amesema.

error: Content is protected !!