December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TCRA kuwezesha wabunifu wapya wa TEHAMA

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari

Spread the love

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na wadau wengine, imeanza utaratibu wa kutoa rasilimali za mawasiliano kwa wabunifu wapya wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), wanaosaidia kutatua changamoto za jamii. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, tarehe 14 Novemba 2022, na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari, katika taarifa yake kwa umma kuhusu programu hiyo.

Dk. Jabir amesema Serikali ya Tanzania imeamua kutoa rasilimali hizo za mawasiliano kwa ajili ya wabunifu kufanya majaribio, ikiwemo misimbo ya rasilimali namba (USSD), zinazotumika kusambaza teknolojia wanazobuni ndani na nje ya Tanzania.

Rasilimali nyingine ni, kikoa (domain) cha dot tz na masafa ya mawasiliano, ambazo awali wabunifu walishindwa kuzipata kutokana na kukosa uwezo wa kumudu gharama zake.

Dk. Jabir amewataka vijana wabunifu na wavumbuzi wa program mbalimbali za kidigitali kujitokeza kwa wingi kupata rasilimali hizo ili waweze kijitengenezea ajira, kuongeza kipato na kutatua changamoto mtambuka za jamii.

“Tumejipanga kuhakikisha wabunifu wapya hasa wa sekta ya TEHAMA wanaoweza kutatua changamoto za jamii yetu wanapata rasilimali hizi za mawaailiano ili washiriki katika uchumi wa kidigitali. Tuna utaratibu wa kutoa rasilimali hizi kwa muda wa miezi mitatu baada ya mbunifu kuidhinishwa na Tume ya Sayansi ya Teknolojia (COSTECH) baada ya kubaini wazo la kibunifu linakidhi kufanyiwa majaribio,” amesema Dk. Jabir.

Dk. Jabir amesema, COSTECH inaendesha program inayojulikana kama Softcenter inayotoa msaada moja kwa moja kwa kampuni changa, kwa ajili ya kutekeleza mpango wa mapinduzi ya kidigitali unaolenga kutatua tatizo la ajira na kukuza ubunifu wenye tija.

“TCRA imeondoa malipo ya ada ya maombi na usajili wa leseni wa rasilimali hizo , kwa wabunifu wenye nia ya kubuni suala lolote litakalorahisisha mazingira ya kawaida ya kila siku ya mwananchi. Wabunifu wanaotaka kutumia fursa hii wanaweza kuwasiliana na dawati la huduma la TCRA au kutembelea tovuti ya mamlaka,” amesema Dk. Jabir.

error: Content is protected !!