TAASISI inayoshughulika na masuala ya maendeleo na ustawi wa jamii (TCE), imezindua kampeni ya malezi chanya, kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo tarehe 18 Julai 2019 jijini Dar es Salaam, Rahim Ndambo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCE amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kutimiza wajibu wao katika kulinda haki za watoto.
Ndambo ameeleza kuwa, TCE imeamua kuanzisha kampeni hiyo, baada ya kubaini ongezeko la vitendo vya ukatili kwa watoto, huku miongoni mwa sababu zinazochochea changamoto hiyo, ni wazazi na walezi, kutotimiza jukumu lao la kulea watoto.
“Lengo la kampeni hii ni kuanzisha jitihada na mkakati endelevu, zenye matokeo, ili kuwafahamisha wazazi,walezi, serikali na jamii kwa ujumla kuwa unyanyasaji huu unatokana na kutokua na malezi chanya katika familia zetu,” amesema Ndambo.
Ndambo ameeleza kuwa, wazazi na walezi wengi nchini wanasahau misingi sahihi ya malezi ya watoto kutokana na kubanwa na majukumu ya kazi, na kuwaacha wafanyakazi za ndani ambao hawana ujuzi wa malezi ya watoto.
“Hatari kubwa imekuwa ikionekana mbeleni, maana vitendo hivi hutokea katika maeneo ya kuaminika na salama kabisa kwa watoto kama nyumbani, shuleni, nyumba za ibada, vyombo vya usafiri na hata kwenye mtandao ya kijamii, kama kutishwa au kushawishiwa ikiwa ni njia ya mtego wa kuweza kuwanasa watoto,” amesema Ndambo.
Marry Mangu, Mratibu wa TCE amesema kampeni hiyo itafanyika katika mikoa 8 iliyoathirika zaidi na vitendo vya unyanyasaji wa watoto.
Mangu ametaja mikoa hiyo ikiwemo, mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Simiyu, Arusha, Kilimanjaro, Tabora na Singida.
Leave a comment