July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TBS yateketeza bidhaa za Marekani

Spread the love

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka Marekani kwa ajili ya msaada katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Musoma kutokana na kutofaa kwa matumizi ya binadamu. Anaandika Eunice Laurian … (endelea)

Shirika hilo pia limeteketeza nepi aina ya Smart Baby zinazotumika mara moja na kutupwa kwa kuwa, hazikidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuisha kwa muda wake wa matumizi.

Akizungumza baada ya bidhaa hizo kuteketezwa katika dampo la Pugu Kinyamwezi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Msemaji wa TBS, Roida Andusamile amesema bidhaa zote zina thamani ya Sh 20 milioni.

Kwa mujibu wa Andusamile, wakati bidhaa zilizoingizwa kwa ajili ya Halmashauri ya Tarime zililetwa zitolewe msaada kwa wahitaji kwenye eneo hilo, na nepi ziliingizwa nchini kwa ajili ya kuuzwa.

Ameitaja kampuni iliyoingiza nepi hizo kutoka China kuwa ni Chaoming & Xlambin Chen, iliyolenga kuzisambaza katika soko la ndani na kwa faida.

Andusamile amesema, “kwa kawaida bidhaa mbalimbali zinapoingizwa nchini kutoka nje kwa ajili ya biashara, kupitia katika mipaka yetu, bandari na viwanja vyetu vya ndege hukaguliwa na maofisa wa udhibiti ubora kutoka TBS, ili kujiridhisha endapo zinafaa kwa matumizi au la.”

Amesema baada ya kukagua mizigo hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam na kupima sampuli kwenye maabara husika za shirika hilo, ulibainika upungufu kadhaa, ikiwemo kwisha kwa muda wa matumizi.

Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Salome Emmanuel ameeleza kuwa, mbali ya muda wa matumizi ya nepi hizo, vipimo vya sampuli za bidhaa hiyo vilionesha kuwa hazifai kutumiwa kwa kuvalishwa watoto kutokana na kuwa na madhara kwa afya zao.

Bidhaa za msaada ambazo watu wa Marekani wanaelezwa kuchanga ili kusaidia wahitaji Tarime, ambazo hata hivyo ziliteketezwa ni losheni za watoto, sabuni za maji kwa ajili ya kunawa mikono, dawa za meno aina ya Colgatte na Crest.

Nyingine ni dawa za kusukutua mdomo ili usinuke, sabuni za kuoshea nywele pamoja na sabuni za maji za kuogea.

Imeelezwa kuwa bidhaa hizo zilibainika mwishoni mwa mwaka jana, na kwamba zilizoingizwa kibiashara ziliteketezwa kwa gharama za kampuni iliyoagiza huku za msaada zikiteketezwa na TBS.

error: Content is protected !!