January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TBS yaongeza nguvu kukabili bidhaa ‘feki’

Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile

Spread the love

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeongeza nguvu katika kupambana na uingizaji wa bidhaa feki nchini kwa kuajiri wafanyakazi 200. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile wakati akizungumza na MwanaHALISI Online katika maadhimisho ya ‘Wiki ya Utumishi wa Umma’ yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Roida amesema, hatua hiyo ni katika kuongeza nguvu kazi katika kukabiliana na uingizaji wa bidhaa feki nchini unaoshamiri kupitia bandari rasmi, bandari bubu na mipaka ya nchi hali ambayo inaathiri afya kwa watumiaji na uchumi wa nchi.

“TBS imekua ikijitahidi kutoa elimu juu ya madhara ya bidhaa feki. Tumezunguka nchi nzima. Hata bandarini tuna watu wetu. Hivi karibuni tutaajiri maofisa 200 ili kuongeza nguvu. Wataanza kazi mwezi wa nane mwaka huu,” amesema Roida.

Ameongeza kuwa, kwa sasa serikali ipo kwenye mchakato wa kupitia watu waliotuma maombi ya kuajiriwa, hivyo ifikapoAgosti mwaka huu watapelekwa katika maeneo yenye uhaba wa watendaji.

Mbali na kuongeza rasilimali watu Roida amesema, TBS itaendelea kutumia Sheria ya Viwango namba mbili ya mwaka 2009 kifungu cha 27 ambayo inatoa adhabu kwa anayethibitika kuingiza na kusambaza bidhaa feki kwa kutozwa faini ya Sh. 50 milioni au kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja na kufutiwa leseni ya viwango na ubora.

“Tunawakaribisha wananchi wafike hapa Mnazi Mmoja kwenye maadhimisho ya Utumishi wa Umma. Tunawapa fursa ya kupata elimu kuhusu shughuli zetu lakini pia na sisi tunapokea maoni yao katika kuboresha huduma zetu,” ameongeza Roida.

Mwezi Machi mwaka huu gazeti la MwanaHALISI Online katika habari yake iliyokuwa na kichwa cha habari “Mabati yasiyokidhi viwango yaingizwa na kusambazwa” lilimnukuu Bitaho Baptister, Mwanasheria wa TBS akisema  “TBS ina changamoto ya uhaba wa watendaji ambapo waliopo sasa ni 230 nchi nzima.”

Hivyo ongezeko hilo la maofisa wapya litalifanya shirika hilo kuwa na jumla ya maafisa 430 nchini nzima ambapo uhaba wa rasilimali watu utakuwa umepungua.

error: Content is protected !!