January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TBS kuondoa bidhaa hafifu sokoni

Spread the love

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa kampeni maalumu ya kuondoa bidhaa hafifu sokoni itakayo tambulika kama Ondoa Bidhaa Hafifu Sokoni. Anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na MwanaHalisi Online jijini Dar es salaam leo, Roida Ndusamile ambaye ni Ofisa Uhusiano TBS amesema kuwa, kampeni hiyo itakuwa ya kushtukiza kwenye masoko ili kubaini wafanyabiashara wanaokaidi agizo la serikali la kuondoa bidhaa hafifu.

“Tuna kampeni ya kuondoa bidhaa hafifu sokoni hasa bidhaa za vilainishi vya mitambo na magari (Lubricants), matairi na nguo za ndani za mitumba,” amesema Ndusamile.

Amesema shirika lilitoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara na jamii juu ya athari za matumizi ya bidhaa hafifu na kwamba, mfanyabiashara atakayebainika anauza bidhaa hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Tunajua wafanyabiashara wanayo taarifa na wanajua kuwa bidhaa hafifu hazihitajiki nchini, wasipoziondoa itakuwa ujeuri sababu elimu wanayo,” amesema na kuongeza;

“Muda wowote kuanzia sasa tutaanza kampeni yetu kwenye masoko, tukikuta bidhaa hafifu sokoni tutaziharibu na muuzaji tutamchukulia hatua za kisheria.”

Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kuwa, bidhaa hafifu zinatoweka na kuwa historia nchini, kampeni hiyo itaanza Dar es salaam na kuzunguka nchi nzima.

Bidhaa nyingine zitakazochunguzwa ubora wake ni nyaya za umeme, umeme nuru (Solar Power) na bidhaa nyingine zinazotumia umeme.

error: Content is protected !!