July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TBC kuonesha bunge ‘live’

Spread the love

KILIO cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge la Tanzania kupitia Shirika la Utangazaji nchini (TBC) ambacho kimekuwa kikitolewa na serikali, sasa kimepata ufumbuzi, anaandika Josephat Isango.

Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF) umeeleza kwamba upo tayari kutoa fedha zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari kupitia TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.

Endapo serikali itakubali ombo hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao vya moja kwa moja vya bunge tofauti na pendekezo la serikali la kunakili baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku.

Ernest Sungura, Mkurugenzi Mtendaji wa TMF leo jijini Dar es Salaam amewaeleza wahariri wa habari na serikali kupitia mwakilishi wake Assah Mwambene ambaye ni Mkurugenzi wa Habari Maelezo kwamba, taasisi hiyo imejipanga kusimamia na kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni kupitia TBC kwa kuyagharamia.

Sungura amesema kwamba miongoni mwa malengo ya mfuko huo ni pamoja na kuleta mabadiliko katika tasnia ya habari pia kuhakikisha wananchi wanapata taarifa.

Januari mwaka huu, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya bunge kupitia TBC.

Miongoni mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh. 4.2 bilioni zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia bunge badala ya kuendelea na kazi ofisini.

Hatua ya serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni huku Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) akilitaka bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya serikali.

Nje ya bunge mjadala huo uliendelea bila kupatikana kwa ufumbuzi ambapo TMF imedhamiria kugharamia matangazo hayo ili kuruhusu wananchi kuendelea kupata matangazo hayo kupitia TBC.

Katika mkutano huo, Mwambene amesema kwamba, serikali itafikiria namna ya kupeleka maombi TMF ya uwezeshwaji katika maandalizi ya miswada miwili ya sheria za habari ili kupitisha sheria zenye matakwa ya wadau.

Kuhusu hilo, Sungura amesema taasisi yake iko tayari kuisaidia serikali kwenye mchakato huo na hata kuitisha kongamano kubwa la wadau.

error: Content is protected !!