Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko TAWA wajitetea madai ya mbunge “udhibiti wanyamapori waharibifu si wetu pekee”
Habari Mchanganyiko

TAWA wajitetea madai ya mbunge “udhibiti wanyamapori waharibifu si wetu pekee”

Mbunge wa Mvomero, Jonas Van Zeeland (CCM)
Spread the love

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema jukumu la udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Mvomero siyo jukumu la mamlaka hiyo pekee bali linatekelezwa kwa ushirikiano na Taasisi zingine za uhifadhi ikiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa Mikumi, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Wananchi wote kwa ujumla.

Pia imewaomba viongozi wa Serikali, wanasiasa na wananchi kwa ujumla kuunga mkono jitihada zinazofanyika na Mamlaka ipo tayari kupokea maoni na ushauri wa kuboresha na kuwatia moyo askari wazalendo wanaokesha mashambani siku zote kufukuza wanyamapori waharibifu hususan tembo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Hayo yamejiri baada ya hivi karibuni kusambaa picha jongefu “video” katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp iliyomhusisha Mbunge wa Mvomero, Jonas Van Zeeland (CCM) akizungumzia suala la uwepo wa tembo katika eneo la Lubungo Wilaya ya Mvomero.

Kipande cha video hicho kilirekodiwa katika Mkutano wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso kilichofanyika katika Kijiji cha Lubungo Wilaya ya Mvomero tarehe 4 Januari, 2023 ambapo pamoja na kutoa maoni yake mbunge huyo alitoa shutuma kwa askari wa TAWA kutofanya kazi ya kudhibiti tembo waharibifu katika Wilaya ya Mvomero.

Akizungumzia tuhuma hizo Afisa Mhifadhi Mkuu-Uhusiano kwa Umma(TAWA), Vicky Kamata kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo tarehe 15 Januari, 2023, amesema TAWA imechukulia maoni hayo kwa uzito mkubwa kwa kuzingatia kwamba yametolewa na muwakilishi wa wananchi.

Amesema kazi ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu inatekelezwa kwa kuzingatia Mkakati wa kitaifa wa kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori wa mwaka 2020 -2024 ambao unaelekeza wadau mbalimbali kushirikiana katika udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.

Kwa muktadha huo, udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Mvomero siyo jukumu la TAWA pekee bali linatekelezwa kwa ushirikiano na Taasisi zingine za uhifadhi. Pili, TAWA kwa kushirikiana na TANAPA na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero maeneo ya kiutendaji yaligawanywa ili kutoa huduma kwa wakati kwa wananchi katika Wilaya ya Mvomero,” amesema.

Amesema TAWA ilipewa kata sita (Lubungo, Melela, Wami Dakawa, Mlali, Mzumbe, Homboza na Songaji). Hifadhi ya Taifa Mikumi ilipewa kata tatu (Doma, Msongozi na Mangae).

Aidha,amesema  Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero alitoa askari wanyamapori ili kushirikiana na askari wahifadhi katika kudhibiti wanyamapori waharibifu hususan tembo.

Afisa Mhifadhi Mkuu-Uhusiano kwa Umma(TAWA), Vicky Kamata

“Katika kukabiliana na changamoto kwenye Wilaya ya Mvomero kwa kipindi cha Oktoba 2020 hadi Desemba 2022 TAWA imefanya jitihada mbalimbali  ikiwamo kufanya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambapo jumla ya siku-watu 3,284 za doria za kudhibiti matukio hayo zilifanyika dhidi ya matukio 264 yaliyotolewa taarifa katika Wilaya ya Mvomero ikiwemo Kata ya Lubungo na Tarafa ya Mlali.

“Pili, takriban watu 4,151 walipewa elimu ya namna bora ya kuepuka madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo,” amesema.

Mengine ni pamoja na kujenga kituo cha askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kikiwa na pikipiki 4 na gari moja katika Kijiji cha Sangasanga kwa ajili ya Askari kufika kwa haraka kwenye matukio kabla tembo hawajaleta madhara.

“Nne, kufuatia uwepo wa matukio katika Kata ya Lubungo, tembo wanne hatarishi walivunwa katika Kijiji cha Lubungo ambapo tembo wawili mwaka 2021 na wengine wawili mwaka 2022,” amesema.

“Tano, kusambaza namba za kupiga simu bure (0800110093) ili kuripoti matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu inayotumika katika Mkoa wa Morogoro.

Ambapo kupitia namba hiyo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2022 miito 48 ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ilipokelewa na kufanyiwa kazi,” amesema.

Amesema TAWA itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ulinzi wa maisha ya watu na mali zao kwa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika vijiji vya Wilaya ya Mvomero na maeneo mengine nchini.

Pia TAWA inatoa rai kwa wananchi kupiga simu za dharura za kuripoti matukio haya na kuacha kuwachokoza au kuwapiga wanyamapori pale wanapowaona katika makazi yao ilikuepuka madhara zaidi kwa wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia awalilia 17 waliofariki ajalini wakisafirisha maiti

Spread the love  RAIS Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa...

Habari Mchanganyiko

Wanawake wachimbaji wajenga zahanati kuokoa afya za wakazi 2000

Spread the love  ZAIDI wakazi 2,000 wa kijiji cha Nyamishiga Kata ya...

Habari Mchanganyiko

Baada ya Congo DR, Somalia mbioni kujiunga na EAC

Spread the love  TAIFA la Somalia liko mbioni kuwa mwanachama rasmi wa...

error: Content is protected !!