July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Tattoo’ zazua mtafaruku sh Dar

Spread the love

 

HOFU imetanda kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtongani, kata ya Kunduchi, Kinondoni, Dar es Salaam nchini Tanzania baada ya wanafunzi wake zaidi ya 30 kuchorwa alama za ‘tattoo’ mabegani na kitu chenye ncha kali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wanafunzi hao wanaoelezwa ni wa darasa la tano, sita na saba wanadaiwa kuchorwa alama hizo kwa nyakati tofauti hivi karibuni na kulazimika kupelekwa zahanati ya Kunduchi kwa uchunguzi wa kiafya.

Taarifa za tukio hilo, zilianza kusambaa mitandaoni zikionesha wanafunzi hao walivyochorwa na mwanafunzi mwenzao anayedaiwa kutumwa na dada wa kazi, kufanya hivyo.

Picha hizo za wanafunzi waliofanyiwa vitendo hivyo, zilikuwa na maelezo kwamba: “Watoto wa shule ya msingi Mtongani wapatao 35 wamechorwa hizo ‘tattoo’ na mtoto mwenzao aliyetumwa na msichana wa kazi.

“Uchunguzi unaendelea ili kujua kwa nini amefanya hivyo na alama ni hizo tu za T na M na hapo wapo zahanati ya Kunduchi wakipima HIV.”

Mwandishi wa MwaanHALISI Online alifika kwenye zahanati hiyo kufuatilia tukio hilo na kupokewa na mhudumu wa kike ambaye hakutaka kutajwa jina akisema: “Ni kweli wanafunzi walikuja hapa kupimwa afya na kwa vile maadili yanatuzuia kutoa taarifa, maelezo zaidi nenda shuleni kwao.”

Mhudumu huyo aliendelea: “Tukio hili lilitokea Jumatatu na wala si leo, na hata hiyo Jumatatu mimi sikuwapo, lakini nilikuja kuambiwa kuwa kuna wanafunzi wamechorwa ‘tattoo’, na walikuja hapa kupimwa kama michoro hiyo imewasababishia madhara kiafya.”

Baada ya maelezo hayo, mwandishi alikwenda shuleni hapo umbali wa kama meta 100, kutoka ilipo zahanati na kukuta askari Polisi wawili waliovalia sare na mwingine kawaida.

Askari hao walikuwa ofisini kwa Mwalimu Mkuu wakifanya naye mahojiano na mwandishi alipoomba kuonana naye, alielezwa na mmoja wa maaskari hao, kwamba asubiri nje kwani kuna dharura.

Wakati mwandishi akiendelea kusubiri nje, alizungumza na baadhi ya wanafunzi wawili waliokuwa nje na kuwauliza kwa nini walijichora na mmoja wao akasema, “si sisi waliojichora ni darasa la tano na la sita“ na kukimbia.

Mwingine alisema, wanafunzi hao wamejichora herufi za majina yao kwa vijiti walivyochonga na kuwa na ncha kali.

Takribani dakika 40 zikiwa zimepita, mwandishi akiendelea kusubiri, zilisikika kelele za mayowe nje, zikitolewa na mwanafunzi wa kike mithili ya anayepigwa. Mwalimu Mkuu akatoka ndani kwenda nje kuangalia kilichotokea.

Mwalimu mkuu aliwaacha walimu wenzake wakishughulikia mwanafunzi huyo aliyepiga mayowe na baadaye wengine watatu kufuatia. Haikufahamika haraka mayowe hayo yalitokana na nini lakini hawakuwa wamepigwa.

Huku tukio hilo likiendelea na walimu kutaka kujua nini kimewasibu wanafunzi wao, Mwalimu Mkuu alimfuata mwandishi alikokuwa amekaa na kumwuliza shida iliyompeleka hapo na mwandishi kumweleza “nafuatilia hili tukio la wanafunzi kujichora ‘tattoo’.”

Mwalimu huyo ambaye hakutaka kujitambulisha, alisema: “Suala hilo liko kwa Mkurugenzi, nenda kwake atakupa taarifa.”

MwanaHALISI Online lilimtafuta Mkurugenzi wa Kinondoni, Hanifa Hamza kwa simu ya mkononi lakini hakupatikana halikadhalika Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

MwanaHALISI Online lilimtafuta Ofisa Elimu Msingi wa Kinondoni, Theresia Kyara saa 12:24 jioni na kumtaka mwandishi kwenda kwa Mkurugenzi na akitoa kibali atakuwa tayari kuzungumza.

Alipoelezwa Mkurugenzi ametafutwa na hapatikani na muda wa kwenda mitamboni unasogea, alisema: “Wewe fika ofisi ya Mkurugenzi, akupe kibali.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema suala hilo wanaoweza kulizungumzia ni ofisa elimu, “sisi tulifika pale kusaidia mamlaka zingine na kuangalia hali ya utulivu inatawala.”

error: Content is protected !!