August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TARI yataka wakulima wa miwa kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti

Spread the love

KITUO cha Utafiti wa mbegu Tanzania (TARI) Kibaha kimewataka wakulima wa miwa kutumia aina nne za mbegu zilizotafitiwa ili kukabiliana na changamoto ya wadudu, magonjwa na ukame katika kuboresha kilimo hicho nchini. Anaripoti Ashura Kazinja, Morogoro… (endelea)

Hayo yalisemwa jana tarehe 1 Agosti, 2022 na Mratibu wa Kitaifa utafiti wa Miwa TARI- Kibaha, Minza Masunga katika  banda la kilimo la Bodi ya Sukari Tanzania lililopo kwenye maonesho ya siku ya wakulima nanenae kanda ya Mashariki yanayofanyika kwenye uwanja Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro.

Alizitaja aina hizo nne za mbegu kuwa ni pamoja na N 47, R 570, TARISCA 1 na 2 ambapo alisema wakulima wa miwa wamekuwa wakitumia mbegu za muda mrefu NCO 376 ambayo imekuwa haina tija kwa kilimo kwao na Taifa kwa ujumla.

Aidha, alisema TARI Kibaha wamekuwa wakifanya utafiti wa miwa ili kuimarisha teknolojia zilizopo na kuongeza mpya na kumfanya mkulima aongeze tija ili uzalishaji wa miwa uongezeke nchini.

Masunga alisema changamoto ya mbegu hiyo ambayo hushambuliwa na wadudu (bacteria) na kuleta udumavu shambani husababisha kushuka kwa asilimia 50 hadi 70 ya sukari kwenye muwa.

Alisema pia mbegu hizo mpya husaidia na kuwa kinzani kwa wadudu na bacteria mbalimbali ikiwemo fungwe (smart) ambao wamekuwa wakipunguza tija ya sukari kwenye muwa kutoka asilimia 70 hadi 100.

Aidha, aliwataka wakulima kutumia mbegu hizo huku wakizingatia kanuni za kilimo ikiwemo kusafisha mashamba na kuhakikisha wanapata tija ya kilimo na kupata tani 80 hadi 100 kwa hekta.

Naye Mkufunzi Mwandamizi kutoka chuo cha Sukari cha Taifa (NSI), Mwanaidi Japhary aliwataka vijana waliomaliza kuanzia kidato cha nne kujiunga na mafunzo ya uzalishaji Miwa ili kuisaidia Serikali kupata wataalamu zaidi na kuweza kuongeza uzalishaji wa sukari na kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.

Naye Meneja wa mafunzo upande wa vipando kutoka Kiwanda cha Sukari Kilombero Tumaini Sawe aliwataka wakulima kutumia mbinu za kisasa za kupanda miwa na kuachana na za kizamani ili kuwa na kilimo bora na kupata tija wakati wa mavuno.

Sawe alisema wakulima wengi wamekuwa wakitumia kilimo cha kizamani cha kuchomeka miwa, mmea ambao baadae hauna tija sababu hauongezi vipando na kuongeza miwa shambani ili kukuza uzalishaji ambapo wakitumia mbinu za kisasa za kupanda miwa ikiwemo ya kulaza miwa ardhini na kuifukia itasaidia kupata vipando vingi baadae na hivyo kuleta tija kwenye kilimo hicho.

error: Content is protected !!