December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yazungumzia uchunguzi kupotea Azory Gwanda

Spread the love

 

MSEMAJI Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amesema Jeshi la Polisi nchini humo, linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio la kupotea kwa aliyekuwa Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Azory Gwanda. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Azory aliyekuwa akifanyia kazi mkoa wa Pwani, akiishia Kibiti, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemva 2017 na mpaka sasa haijulikani yupo wapi.

Msigwa amejikuta akizungumzia suala hilo baada ya kuulizwa swali leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021 na Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari mkoani Mwanza, Edwin Soko.

Ni katika mkutano wa Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kutoa taarifa ya wiki ya utendaji kazi wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tangia kupotea Azory hakuna ripoti maalum ya Serikali, tunaamini Serikali ni sikivu na inamiliki vyombo vya ulinzi na usalama, angalau ingeweza kuja na majibu na ripoti malum ili kuonesha status ya azory hadi kufikia sasa katika kufikia uwajibikaji,” ameuliza Soko.

Soko amesema, “hii itasaidia sana taifa letu libaki katika jicho salama dhidi ya majukwaa mbalimbali ya kimataifa.”

Akijibu swali hilo, Msigwa amesema, “Polisi wameshatoa taarifa na wanaendelea kufanya uchunguzi, sababu Polisi wanajukumu kufanya uchunguzi na hawafanyi kwa Azory peke yake, wanafanya kwa watu wote wanaopata madhila kama hayo ya kupotea, kufariki dunia na matatizo yote.”

Msigwa amesema, Jeshi la Polisi litakapokamilisha uchunguzi wake dhidi ya tukio hilo, litatoa taarifa.

“Ninachoomba tuendelee kuwasikiliza Polisi, watatuambia nini juu ya hatma ya wanayoendelea kufanya ya kulichunguza jambo hili na baadae watatuambia uchunguzi wao utakapokamilika, nini wamekiona na tutajua cha kufanya. Lakini sasa hivi hakuna ripoti imeandaliwa maalum ya Azory zaidi ya uchunguzi unaofanywa na Polisi,” amesema Msigwa.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni akielezea jinsi mmewe alivyotoweka alidai, asubuhi ya tarehe 21 Novemba 2021, watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika Kibiti, alipokuwa Azory na kumchukua.

Mbali na swali hilo, Soko alihoji Serikali imefikia hatua gani katika utekelezwaji wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Sheria ya Afrika Mashariki dhidi ya kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo kupinga baadhi ya vifungu yvya Sheria ya Huduma ya Habari ya 2016.

“Katika kesi namba 2/2017 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki, mahakama ilitoa hukumu kwambas sheria ina ukakasi katika vifungu 12, nini utayari wa Serikali kutekeleza hukumu hiyo mpaka sasa,” ameuliza Soko.

Akijibu swali hilo, Msigwa amesema Serikali haijatekeleza hukumu hiyo kwa kuwa kuna masuala ya kimahakama yanaendelea.

“Kwenye kesi ya Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna rufaa illikuwa imeandaliwa, kwa hiyo hili suala liko kisheria, nisingependa kuzungumzia hapa. Mambo yatakapokuwa tayari kwa ajili ya kuzungumzia nje tutayazungumzia,” amesema Msigwa na kuongeza:

“Lakini sio kwamba Serikali imepuuza, hapana. Isipokuwa kuna masuala ya kimahakama yanaendelea.”

Kesi hiyo Na. 2/2017, ilifunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Ambapo kupitia hukumu ya mahakama hiyo, Serikali ilitakiwa kurekebisha vifungu 12 vya sheria hiyo vilivyodaiwa kwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

error: Content is protected !!