November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yazitengea benki trilioni 1 zishushe riba

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga Sh.1 trilioni kwa ajili ya mikopo kwa mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu ili mabenki na taasisi hizo zitoe mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

“Serikali imeendelea kulegeza masharti ya uanzishwaji wa ofisi za wakala wa mabenki, kushusha riba inayolipwa kwa akaunti za fedha za mitandao pamoja na kutenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu ili mabenki na taasisi hizo zitoe mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 12 Novemba 2021, wakati akiahirisha mkutano wa tano wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Februari mosi, mwakani. Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2022/2023.

Akizungumzia kuhusu, riba kubwa za mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha, Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti kupitia Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo kupunguza kiwango cha akiba kinachowekwa na mabenki katika Benki Kuu.

”Hatua hizo zinalenga kupunguza kiwango cha riba kwenye mikopo ya mabenki ya kibiashara na taasisi za fedha, kupunguza riba katika shughuli za kilimo kwa kiwango kisichozidi asilimia 10 na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi ili kuchechemua shughuli za kiuchumi.

”Licha ya hatua hizo, bado kumekuwa na changamoto ya kutoshuka kwa kiwango cha riba kinachotozwa na mabenki na taasisi za fedha. Kwa mantiki hiyo, ninaiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ikutane na taasisi za fedha nchini kuona namna wanavyoweza kupunguza riba kubwa kwenye mikopo wanayotoa hususan kwa makundi ya wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.”

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ishirikiane na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inatekeleza vema Mpango wa Serikali wa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wakandarasi wa ndani pamoja na kuendelea kulipa madeni ya wazabuni kwa wakati.

error: Content is protected !!