SERIKALI ya Tanzania, imeweka misimamo kuhusu mkutano wa 26 wa mabadiliko ya tabia ya nchi , unaotarajiwa kufanywa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 12 Desemba 2021, jijini Glassgow nchini Scotland. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).
Msimamo huo umetangazwa leo tarehe 11 Oktoba 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo, akizungumzia maandalizi ya mkutano huo.
Jafo amesema msimamo wa Tanzania utawekwa katika masuala saba, yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo, ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba na makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi.
Amesema, msimamo wa Tanzania ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutekeleza ahadi yake ya kutoa fedha dola za Marekani 100 bilioni , kila mwaka hadi ifikapo 2025, kwa ajili ya kuziwezesha nchi zinazoendelea kuweka mipango mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Jafo amesema, msimamo mwingine wa Tanzania katika mkutano huo, ni sekta ya kilimo kutoingizwa katika sekta zinazotakiwa kuounguza gesi joto kwa kuwa inaathirika na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kumekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea, kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo, katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto. Mchango wa uzalishaji wa gesi joto utokanao na shughuli za kilimo, ni mdogo katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea,” amesema Jafo.
Pia, Jafo amesema Tanzania imeweka msimamo katika masuala ya uendelezaji na usambazaji teknolojia, ambao unazitaka nchi zilizoendelea zihakikishe nchi zinazoendelea zinapatiwa teknolojia hizo kwa gharama nafuu na uwazi.
“Makubaliano ya Paris yanazitaka nchi zilizoendelea kuziwezesha nchi zinazoendelea kutumia teknolojia mpya na za kisasa,”
“Ambazo zitasaidia kuongeza uwezo wa nchi hizo kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza uzalishaji wa gesijoto, kwa kuwa Teknolojia hizo ni ghali na hazipatikani kirahisi,” amesema Jafo.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Jafo amesema, utaiwezesha Tanzania kufaidika na fursa mbalimbali kama msaada wa fedha na teknolojia.
“Kama nilivyoeleza, athari za mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini kwa sasa ni moja ya changamoto zinazolikabili taifa letu kiuchumi, kijamii na ustawi wa watu wetu,” amesema Jafo na kuongeza:
“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu ni muhimu, kwa vile utaiwezesha Tanzania kufaidika na fursa mbalimbali kama vile upatikanaji wa fedha na teknolojia, zitakazosaidia katika juhudi za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.”
Leave a comment