October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yashtakiwa kesi 13, yadaiwa dola 185 milioni

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi

Spread the love

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amebainisha kuwa, mashauri 13 yenye jumla ya madai kiasi cha dola za Marekani 185.5 Milioni, yamefunguliwa dhidi ya serikali katika mahakama za kimataifa za usuluhishi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo tarehe 9 Novemba 2018, Prof. Kabudi amesema kesi hizo zimefunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya London (LCIA), Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) na Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA) kuanzia mwezi Novemba 2015 hadi mwaka huu.

“Mashauri yaliyofunguliwa nje ya nchi dhidi ya serikali kuanzia Novemba 2015 ni 13, aidha mashauri hayo yapo katika mahakama mbalimbali za usuluhishi ikiwemo (PCA), (LCIA) NA (ICSID) na huko Johannesburg Afrika Kusini. Jumla ya madai ya kesi hizo ni dola za kimarekani 185,580,009.76,” amesema Prof. Kabudi.

Aidha, amesema mashauri yote yaliyopo kwenye mahakama za kimataifa bado hayajatolewa uamuzi, hivyo takwimu halisi za madai na gharama ambazo serikali inaweza kuwajibika kulipa itapatikana baada ya mashauri husika kukamilika na uamuzi kutolewa.

Prof. Kabudi ametoa takwimu hizo akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliyetaka kujua tangu mwaka 2015 hadi sasa Tanzania imefunguliwa mashauri mangapi katika mahakama za kimataifa kuhusiana na masuala ya uwekezaji na mikataba ya kibiashara.

error: Content is protected !!