July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yashika nafasi ya 22 kwa TB

Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Dornad Mmbando

Spread the love

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Dornad Mmbando, amewataka wananchi kushiriki katika tiba shirikishi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) zitolewazo nchini. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Wito huo unatolewa ikiwa imebaki siku moja kufikia kilele cha maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 1.5 hufariki kwa ugojwa huu kila mwaka duniani.

Akizungumza na waandishi leo ofisini kwake, Mmbando amesema, asilimia kubwa ya vifo hivyo hutokea barani Afrika hususani kusini mwa jagwa la Sahara huku Tanzania ikishika nafasi ya 22 duniani kwa wagojwa wa kifua kikuu.

Amesema, watu milioni 9 duniani wanaugua kifua kikuu na kati yao wanaoishi katika mazingira magumu na umaskini. Makundi yanayoathirika zaidi kwa kupata ugonjwa wa kifua kikuu ni pamoja na  waathirika wa virusi vya ukimwi, watoto, wazee, wafugwa na watu wenye  magojwa ya muda mrefu kama saratani na kisukari.

Mmbando amesema, Tanzania inashika nafasi ya 6 barani Afrika, na mikoa inayoongoza kwa ugojwa huo ni, Mbeya, Mara, Shinyanga, Tanga, Mwanza, Arusha, Morogoro na Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa, zaidi ya asilimia 30 ya vifo vya watu walioathirika na Ukimwi vinatokana na kifua kikuu. Hivyo mtu anapokuwa ameathirika ni lazma apime virusi vya ukimwi.

“Kuna dalili ambazo zinafahamika sana ambazo mtu akiziona ni lazima aende hospitali kufanya uchunguzi ambazo ni kukohoa kwa wiki mbili mfulilizo, homa za mara kwa mara, kutokwa jasho usiku, kukosa hamu ya kula na kupungua uzito kupita kiasi,” amesema Mmbando.

Aidha, Mmbando amesema, kuna aina mbili za kifua kikuu, cha mapafu na nje ya mapafu, ambacho mtu mwenye kifua kikuu cha mapafu anaweza  kuambukiza karibu watu 10 kwa wakati mmoja, kwa njia ya hewa wakati anapokohoa au kupiga chafya.

Mmbando ametoa wito kwa wananchi wote mara waonapo dalili hizo waende hospitali mapema kwa ajili ya uchunguzi wa kina ili kuwahi matibabu kwani unatibika ukiwahiwa.

Amesema dawa zinapatikana katika vituo vyote vya afya, hospitali binafsi na za serikali na zinatolewa bure.

error: Content is protected !!