December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yapiga ‘stop’ ndege za Kenya

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imezuia ndege za Shirikla la Ndege la Kenya (KQ) kutua nchini humo kuanzia leo Jumamamosi tarehe 1 Agosti 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zuio hilo limetolewa jana Ijumaa tarehe 31 Julai 2020 na Hamza Johari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Kwa mujibu wa taarifa ya TCAA, ndege za Kenya hazitaruhusiwa kutua katika viwanja vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar vya Tanzania hadi hapo baadaye itakapotolewa taarifa nyingine.

TCAA imeeleza, Serikali ya Tanzania imebaini kupitia vyombo vya habari kwamba raia wake wametengwa katika orodha ya watu watakaoruhusiwa kuingia Kenya, baada ya nchi hiyo jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufungua anga lake kuanzia leo Jumamosi.

Hamza Johari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imebaini kupitia vyombo vya habari kutengwa kwake ndani ya orodha ya nchi ambazo watu wao wataruhusiwa kwenda Kenya kuanzia tarehe 1 Agosti 2020, tarehe ambayo Kenya itafungua anga lake kwa safari za kimataifa tangu iliposimamisha tarehe 25 Machi 2020,” inaeleza taarifa ya TCAA.

Hatua hiyo ya TCAA kuzuia ndege za Kenya kutua katika viwanja wa Tanzania, imekuja baada ya Serikali ya Kenya kuitenga Tanzania, katika orodha ya mataifa yatakayoruhusiwa kuingia nchini humo.

James Macharia, Waziri wa Usafirishaji wa Kenya, jana Ijumaa alitaja orodha ya mataifa 11 ambayo raia wake wataruhusiwa kuingia nchini humo, kwa maelezo kwamba, yamefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Virusi vya Corona (Covid-19).

Nchi hizo ni, China, Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Switzerland, Uganda, Rwanda, Namibia na Morocco.

Hata hivyo, Macharia alisema, Serikali ya Kenya inaendelea kufuatilia kwa ukaribu mataifa mengine kwa ajili ya kuongeza idadi ya mataifa yatakayoruhusiwa kuingia nchini humo.

error: Content is protected !!