August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yanufaika na madaktari wa Cuba

Spread the love

MBUNGE wa Gando, Othman Omar Haji (CUF) ameihoji serikali kueleza namna Tanzania ilivyofaidika na utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano baina yake na Serikali ya Cuba, anaandika Dany Tibason.

Swali la mbunge huyo lililenga hasa kutaka kujua faida ya ushirikiano huo kwa Tanzania kwenye eneo la sekta ya afya.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala amesema serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea madaktari bingwa kutoka Cuba ambao wanapangiwa kufanya kazi katika Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Rufaa Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

“Madaktari hawa wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za kibingwa kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari wanaofanya nao kazi katika hospitali hizo,” amesema Dk. Kigwangala.

Pia amesema kwa kushirikiana na kampuni ya Labiofarm ya Cuba, serikali ya Tanzania imefanikiwa kujenga kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kibaiolojia kwa ajili ya kuua viluilui vya mbu waenezao malaria.

Amesema serikali iligharimia ujenzi wa kiwanda hicho huku serikali ya Cuba ikitoa msaada wa wataalamu.

“Ni matarajio yetu kuwa wataalamu hao watawajengea uwezo Watanzania ili waweze kutengeneza bidhaa hizo bila ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi kwa siku zijazo,” amesema.

Dk. Kigwangala amesema viuadudu hivyo vimeanza kutengenezwa kuanzia Desemba mwaka jana na kwamba kwa sasa uhamasishaji wa Halmashauri mbalimbali kununua bidhaa hizo umeanza.

Alisema iwapo viuadudu hivyo vitatumika vizuri, vitasaidia kupunguza mbu waenezao malaria na hivyo kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini.

error: Content is protected !!