January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yang’ang’aniwa utekelezaji mapendekezo ya UN

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Spread the love

 

MASHIRIKA Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), yanayoshughulika na masuala ya utetezi wa haki za binadamu, yameiomba Tanzania, ibadilishe msimamo wake wa kutoyafanyia kazi baadhi ya mapendekezo iliyopewa na Umoja wa Mataifa (UN), ambayo hayana ukakasi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 7 Desemba 2021, jijini Dar es Salaam na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) na Shirika la Save the Children.

Katika kikao kazi cha kuchambua mapendekezo 252, yaliyotolewa na Baraza la Haki la UN, Novemba 2021, katika kikao cha tatu cha Baraza la Haki la Umoja UN, cha tathmini ya mapitio ya hali ya haki za binadamu (UPR), kilichofanyika nchini Uswis.

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, ameiomba Serikali iyatizame upya mapendekezo 132 kati ya 252 (52%), ambayo haijakubali kuyatekeleza.

Olengurumwa amesema, tangu Tanzania ifanyiwe mapitio kiwango chake cha kukubali kufanyia kazi mapendekezo inayopewa katika baraza hilo, kimeshuka kutoka asilimia 70 mwaka 2011, hadi kufikia asilimia 43 mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju

“Tanzania imefanyiwa mapitio mara tatu, mara ya kwanza 2011 ambapo tulitekeleza mapendekezo sawa na asilimia 70. 2016 tulipokea mapendekezo 227, kati ya hayo ilikubali 133, sawa na asilimia 58. 2021 tumeshuka kidogo tuko asilimia 43,” amesema Olengurumwa.

OIengurumwa amesema “hii trend (mwenendo)tuirekebishe kwa kupanda, badala ya kushuka na tunaweza ipandisha hadi Februari 2022 itakuwa bora zaidi.”

Olengurumwa ametaja baadhi ya mapendekezo ambayo Tanzania haijaonesha nia ya kuyatekeleza, ikiwemo yanayohusu haki za kijamii (2), haki za wafugaji (1), uhuru wa kujieleza (18), haki za binadamu na mikataba ya kimataifa (60).

Mengine ni haki za kiuchumi (13) na mapendekezo kuhusu haki za asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu (9).

Mratibu huyo wa THRDC, amechambua mapendekezo yanayohusu haki za kiraia na kisiasa, ambayo Serikali haijaonesha nia ya kuyatekeleza, ikiwemo haki ya kupata dhamana na kutowekwa rumande kinyume cha sheria.

Mengine ni ufutwaji adhabu ya kifo na nchi kuridhia mikataba ya kimataifa inayolenga kukomesha utesaji binadamu na ulinzi dhidi ya kupotezwa.

Naye Afisa Uchechemuzi kutoka LHRC, Raymond Kanegene, amesema kuna mapendekezo mengine ambayo Tanzania haijaoneshania ya kuyatekeleza, yanahitaji kutekelezwa kutokana na umuhimu wake.

“Natoa wito katika yale mapendekezo ambayo yamewekwa kando, kuona namna gani Serikali na wadau tunayafanyiaje kazi kwa undani, kuna mengine tunaona yamewekwa kando yana uhitaji wa kufanyiwa kazi,” amesema Kanegene.

Akijibu maombi hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, amesema Serikali ya Tanzania imeishia kuyaona mapendekezo hayo, kwa kuwa yanakwenda kinyume na misingi ya katiba, sheria na mila za nchi.

“Yapo baadhi ukiyaangalia yanakinzana na katiba, sheria, taratibu, kanuni, mila na imani zetu. Mathalani yapo yaliyohusu adhabu ya kifo yaondolewe, utakuta tumeyaona. Yapo yaliyoongelea ubakaji ndani ya ndoa, kwa mila na tamaduni zetu mke wangu naambiwa nimebaka? Tumeona tuweke pembeni,’ amesema Mpanju.

Mpanju amesema “tumeona ushoga na usagaji, haya hatuwezi kuyakubali, no (hapana). Tumeona mikataba tukiyaridhia yataenda kinyume na nchi yetu tumesema no.”

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Katiba na Sheria, amesema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo ambayo hayatakinzana na sheria za nchi.

Mpanju amesema, Serikali itawasilisha rasmi mapendekezo iliyokubali kuyatekeleza katika baraza hilo, Februari au Machi 2022.

error: Content is protected !!