October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yakubali mapendekezo 167 ya UN

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imekubali kutekeleza mapendekezo 167, kati ya 252 yaliyowasilishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), yenye malengo ya kukuza na kulinda haki za binadamu nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mapendekezo hayo yalikubaliwa jana tarehe 23 Machi 2022, jijini Geneva Uswis, katika mkutano wa 49 wa Baraza la Haki za Binadamu la UN, wa mapitio ya hali ya haki za binadamu duniani (UPR), ambao ulirushwa mubashara na chaneli ya YouTube ya umoja huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene, alisema Tanzania imekubali kutekeleza mapendekezo hayo 167, kwa kuwa yanakidhi matakwa ya Katiba ya nchi, mila na tamaduni za Watanzania.

“Mapendekezo 167 yaliyokubaliwa ni yale yanayofuata katiba ya Tanzania na ya Zanzibar. Pia yanawiana kwa ajili ya kukuza na kulinda haki za kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na masuala yanayojitokeza ya haki za binadamu na rushwa,” alisema Simbachawene.

Simbachawene alisema, mbali na Tanzania kukubali kutekeleza mapendekezo 167, imekubali kutekeleza kwa sehemu mapendekezo 20, huku ikiyaona mengine 65.

“Kutokana na matokeo ya mashauriano mapana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikubali kutekeleza mapendekezo 187, ambapo mapendekezo 20 yamekubaliwa kwa sehemu. Pia, Tanzania imeona mapendekezo 65,” alisema Simbachawene.

Simbachawene aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa, Serikali ya Tanzania na Zanzibar, zitayafanyia kazi mapendekezo hayo, pia itayasambaza kwa watendaji wa Serikali, taasisi zisizo za Serikali za haki za binadamu na asasi za kiraia.

error: Content is protected !!