October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania yaanzisha maabara mpya ya corona

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imeanzisha maabara mpya ya kupima ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo ya Serikali ya Tanzania kuanzisha maabara mpya, imekuja kufuatia dosari zilizojitokeza katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, katika ukusanyaji pamoja na upimaji wa sampuli za Covid-19.

Dosari hizo zilibainishwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli tarehe 3 Mei 2020, siku kadhaa baada ya nchi ya Tanzania kusimama kutoa takwimu za mwenendo wa Covid-19.

Mara ya mwisho takwimu za mwenendo wa Covid-19 Tanzania Bara, zilitolewa tarehe 29 Aprili 2020, na Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu, wakati  Zanzibar mara ya mwisho kutoa takwimu za ugonjwa huo, ilikuwa tarehe 7 Mei 2020.

Mnamo tarehe 8 Mei 2020, Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, alisema takwimu hizo zitaanza kutolewa tena, pindi maabara hiyo itakapofanyiwa marekebisho.

Leo Jumamosi tarehe 23 Mei 2020, Waziri Ummy amekagua maabara hiyo mpya yenye uwezo wa kupima sampuli  1,800 za Covid-19, ndani ya saa 24, iliyojengwa maeneo ya Mabibo jijini Dar es Salaam.

“Upimaji wa Sampuli zote za Covid-19 umehamishiwa katika maabara mpya iliyokamilika kujengwa katika eneo la Mabibo Dar es Salaam ambayo kwa sasa ndiyo itakuwa maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii,” amesema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy, maabara hiyo imeanza kazi leo, baada ya kuwapima Covid-19 madereva wa malori.

Waziri Ummy aliwahakikishia madereva hao kwamba, watapata majibu yao ndani ya saa 24.

error: Content is protected !!