May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania, Saudi Arabia kukuza ushirikiano wa kibiashara, utalii

Spread the love

 

NCHI ya Tanzania na Saudi Arabia, zimeahidi kukuza ushirikiano katika biashara ya mazao ya kilimo pamoja na utalii. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ahadi hiyo ilitolewa jana tarehe 25 Mei 2021, katika mazungumzo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwana wa Kifalme Faisal Farhan Al Saud, yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Samia alimuahidi , Mwana wa Kifalme Faisal kwamba, Serikali yake ipo tayari kukuza uhusiano na ushirikiano wake na Saudi Arabia.

“Rais Samia amemtaka kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia, Mtukufu Salman bin Abdulaziz Al Saud na kumhakikishia kuwa, Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Saudi Arabia, katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na ustawi wa jamii,” ilisema taarifa ya Msigwa.

Taarifa ya Msigwa ilitaja baadhi ya maeneo ambayo Rais Samia ameomba kushirikiana na Saudi Arabia, ni uimarishaji biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi, mazao ya kilimo, kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania na kuanzisha ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Saudi Arabia Visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwana wa Kifalme Faisal alimhakikishia kwamba Saudi Arabia ipo tayari kuimarisha uhusiano huo, katika maeneo mbalimbali yakiwemo biashara na uwekezaji.

“Mwana wa Kifalme Faisal, amebainisha kwamba ni muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia, kushirikiana ili kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili, ikiwa ni pamoja kuwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia, ili kukuza utalii na biashara,” ilisema taarifa ya Msigwa.

error: Content is protected !!