May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania, Msumbiji mguu sawa kudhibiti ugaidi

IGP, Simon Sirro (kushoto) akisalimiana na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi la Msumbiji, Bernadino Rafael walipokutana mkoani Mtwara kwa mazungumzo

Spread the love

JESHI la Polisi Tanzania na Msumbiji,  yametangaza operesheni ya kusaka kundi linalofanya uhalifu katika mpaka wa mataifa hayo mawili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mtwara … (endelea).

Hayo yamesemwa jana  Ijumaa tarehe 20 Novemba 2020 na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi la Msumbiji, Bernadino Rafael baada ya kufanya mazungumzo na Insepekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro mkoani Mtwara.

Akizungumzia kikao kazi hicho, Kamanda Rafael alisema, majeshi hayo mawili yatafanya operesheni ya pamoja ili kutokomeza kundi hilo la uhalifu.

“Tutafanya operesheni pamoja, tutafanya kubadilisha taarifa pamoja kati ya Msumbiji na Tanzania. Kama tunajua watu wanaingia nchi yetu kama wauaji wanatoka Msumbiji wanakuja huko sisi tufunge mpaka,” alisema Kamanda Rafael.

Kamanda Rafael alisema “Polisi wa Msumbiji na Tanzania tutaweza kufanya bidii kwa kushirikiana na wananchi na sisi tumeungana kufanya kazi pamoja.”

Aidha Kamanda Rafael amewaomba wananchi waishio mpakani kutoa taarifa za watu wasiojulikana.

“Tumeongea mambo ya kufanyia kazi pamoja katika mpaka,  tufanye kazi na wananchi wanaoishi mpakani sababu kila wakati wanapoona mtu hawamfahamu tuwaambie jeshi,” amesema Kamanda Rafael.

Kwa upande wake, IGP Sirro amesema wamekubaliana namna majeshi yao yatakavyoshirikiana kukabiliana na Genge hilo la uhalifu.

“Tumefanya mszungumzo pia alikuja kuona matukio yaliyotokea  kwa watu waliotoka Msumbiji waliovamia Kitaya na vijiji vingine. Tumezungumza na kukubaliana mambo ya kufanya. Namna majeshi yetu yatashirikiana kukabiliana na wahalifu,” amesema IGP Sirro.

IGP Sirro alisema waliohusika na matukio ya utesaji raia na uharibifu wa mali zao wanachukuliwa hatua.

“Wananchi wetu wamepata shida na waliofanya shida lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria zetu kwa kushirikiana na Msumbiji sababu wana taarifa watu wanaotoka huko kuja kufanya Tanzania,” amesema IGP Sirro.

Aidha, IGP Sirro aliwataka wananchi waliokimbia makazi yao katika maenei ya mpakani warudi kwa kuwa Jeshi limejipanga kulinda usalama wao.

“Kimsingi ni kwamba, tumejipanga vizuri wananchi wetu waendelee kurudi kwenye yale maeneo waliyokimbia kule mpakani (mpakani mwa Tanzania na Msumbiji).  Waendelee kurudi sababu majeshi yetu yako imara,” amesema IGP  Sirro.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania alisema, tatizo hilo halitachukua muda mrefu kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kutokomeza uhalifu huo.

IGP Sirro alisema Jeshi la Polisi litachukua muda mfupi kukabiliana na uhalifu huo, kama ilivyofanya katika kukabiliana na mauaji ya raia katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani.

“Tumeshajiimarisha, tutahakikisha hili tatizo litachukua muda mfupi kama ilivyokua kwenye tatizo la Kibiti na Ikwiriri ilivyochukua muda mfupi. Hawa wahalifu tutawashughulikia huko huko waliko,”

“Niwahakikishie kwamba hili tatizo litachukua muda mfupi, hawa wahuni tutawashughilikia ikiwezekana kwa makubaliano tutawashughulikia huko huko walipo,”  amesema IGP  Sirro.

error: Content is protected !!