RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake inataka kuifanya Tanzania kuwa kituo cha matibabu ya afya ya kibingwa kwa nchi inazopakana nazo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).
Akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni, Kigoma, leo Jumanne, tarehe 18 Oktoba 2022, Rais Samia amesema ili kufanikisha lengo hilo, Serikali yake imetenga kiasi cha Sh. 5 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Kanda mkoani humo.
“Kama nilivyosema Kigoma ni mkoa wenye watu wengi lakini uko pembezoni mwa Tanzania umepakana na nchi jirani na sisi maono yetu tuwe na utalii wa afya, watu watoke nchi jirani wapate matibabu. Tanzania iwe kituo cha ubingwa wa mambo ya afya kwa nchi tunazopakana nazo,” amesema Rais Samia.
Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni, Rais Samia amesema Serikali yake itapeleka Sh. 2 bilioni, kwa ajili ya kumalizia majengo yaliyobakia ili hospitali hiyo ikamilike.
Aidha, Rais Samia amesema hospitali hiyo inatarajia kuanza kutoa baadhi ya huduma ikiwemo ya vipimo vya CT-Scan, kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu.
Amesema upanuzi wa hospitali hiyo utasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, pamoja na kuokoa fedha ambazo ilikuwa inatumia kufuata huduma katika Hospitali nyingine kubwa.
Leave a comment