July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania kuongoza Afrika Mashariki katika mawasiliano

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akiwa na Naibu wake, Januari Makamba

Spread the love

JUMLA ya Dola za Marekani Milioni 170 na Sh. Bil 17.71 zimetumiwa katika uwekezaji kwenye ujenzi wa mkongo wa taifa katika awamu ya kwanza na ya pili. Anaadika Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Igalula, Mhandisi Athumani Mfutakamba (CCM).

Mhandisi Mfutakamba alitaka kujua serikali imejiandaaje kifedha ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kuongeza biashara za matumizi ya kompyuta

 Prof. Mbarawa amesema, baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa mkongo wa taifa, serikali imeanza kutekeleza hatua ya kwanza ya mradi wa mkongo wa taifa awamu ya tatu.

Amesema, lengo wa uwekezaji huo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano katika Kanda ya Afrika Mashariki kama ilivyoelezwa katika Sera ya Teknolojia ya Habari na Wawasiliano (TEHAMA) yamwaka 2003.

Prof. Mbarawa amesema, katika awamu ya tatu ya mradi wa mkongo wa taifa jumla ya Dola za Marekani Milioni 93.7 na Sh. bilioni mbili zitawekezwa katika ujenzi wa mtandao na kituo cha kutunzia kumbukumbu kitakachowezesha kumbukumbu kuhifadhiwa hapa nchini hivyo kurahisisha matumizi ya TEHAMA.

Amesema, kukamilika kwa awamu mbili za mkongo wa taifa wa mawasiliano kumeijengea nchi heshima kubwa kwa majirani zake ikiwemo nchi hizo kutumia mkongo huo katika mawasiliano ya kimataifa kupitia mikongo ya baharini ya SEACOM na EASSY.

Akiendelea kujibu maswali hayo ametaja nchi ambazo tayari zinatumia mkongo wa taifa na kuiingizia serikali mapato ni pamoja na Zambia, Shelisheli, Malawi, Rwanda, Burundi na Kenya, ambapo Uganda inaendelea na ujenzi wa mkongo ili kufikia Mutukula na kuunganisha na mkongo wa Tanzania ili nchi hiyo ianze kuutumia kwa ajili ya mawasiliano ya kimataifa.

Kuhusu ujenzi wa kituo cha kuhifadhia kumbukumbu , waziri huyo amesema, kitaruhusu utunzaji wa kumbukumbu hapa nchini pamoja na nchi jirani zitakazopenda kufanya hivyo.

Aidha, serikali ilitenga sh. bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa kijiji cha TEHAMA kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na mwaka 204/2015 zimetengwa Sh. bilioni 2.5, ambapo kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano katika kanda ya Afrika Mashariki.

error: Content is protected !!