January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanzania haitaandika Katiba Mpya

Kaimu Mwenyekiti wa JUkwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda

Spread the love

KATIBA Mpya inayotokana na maoni ya wananchi, tayari imeshindikana. Bunge Maalum la Katiba, limeshindwa kufanya kazi iliyotumwa. Limeishia mivutano, malumbano, kejeli, vijembe, matusi, ubaguzi na mipasho, anaandika Pendo Omary.

Yote hayo yamebarikiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samwel Sitta.

Hebron Mwakagenda, makamu mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) amesema, Sitta amewanyima wananchi fursa muhimu ya kujiandikia katiba yao.

“Kuwepo kwa wabunge na wawakilishi ndani ya Bunge Maalum, kulikinzana na dhana ya katiba kama zao la wananchi wenyewe. Wawakilishi na wabunge wamechochea sana kuvunjwa kwa dhana kuwa katiba, ni mkataba mkuu kati ya watawala na wananchi,” ameeleza Mwakagenda.

Amesema, “Bunge na Baraza la Wawakilishi ambavyo ni vyombo toto vya Katiba, havikuwa na mamlaka ya kuzaa katiba.”

Aidha, kitendo cha Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201 na kususia bunge hilo ni pigo kubwa kwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya nchini.

Kitendo cha kupindishwa kwa Kanuni za Bunge Maalum katika hatua ya uzinduzi; jambo ambalo limesababisha rasimu ya Katiba kuwasilishwa bungeni kabla ya Bunge kuzinduliwa, ni ishara kuwa kulikuwa na hila za serikali juu ya mchakato huu.

Ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, Jaji Frederick Werema ukupingana na ule uliotolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, juu ya mamlaka ya Bunge Maalum.

Othuman alisema, Bunge Maalum halina mamlaka ya kugeuza rasimu ya katika kutoka muundo wa serikali tatu hadi mbili zinazopigiwa chapuo na CCM.

Badala ya kutafuta suluhu, maoni ya Othman yalinyamaziwa au kubezwa; hali iliyomfanya Othman kujiengua kutoka kamati ya uandishi.

Othman ni miongoni mwa wajumbe waliopiga kura ya hapana katika Katiba Inayopendekezwa.

Lakini badala ya kuheshimu haki yake ya kupiga kura kwa utashi wake, liliibuka wimbi la kidikteta la ndani ya chama tawala kumshambulia na kumdhihaki. Hatimaye Othuman alifutwa kazi.

“Badala ya Katiba Mpya kuwa chanzo cha maridhiano, muafaka na maelewano, imeishia kuwa zao la uhasama. Kwa sababu hiyo na nyingine, Katiba inayopendekezwa haiwezi kuitwa Katiba Mpya,” ameeleza Mwakagenda.

Ni vema wananchi wasome na kuelewa Katiba Inayopendekezwa na kuilinganisha na Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 (2005) na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (2010).

Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi imeshindwa kupatikana, kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alijiingia katika mradi huu bila maandalizi na utashi wa kisiasa.

Alijiingiza katika utafutaji wa katiba mpya kwa kusukumwa na mvumo wa wanasiasa wa upinzani, vyombo vya habari na wanaharakati wengine. Ndiyo sababu hivi sasa ameungana na chama chake kupuuza maoni ya wananchi katika kutunga katiba mpya.

error: Content is protected !!