Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Tanzania Bara, Zanzibar kufumua sheria za habari
Habari Mchanganyiko

Tanzania Bara, Zanzibar kufumua sheria za habari

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia
Spread the love

 

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeahidi kushirikiana katika kuzifanyia marekebisho sheria zinazosimamia sekta ya habari nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 9 Machi 2022, Visiwani Zanzibar, katika mkutano wa sita wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Ni baada ya Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, kuomba sheria zinazosimamia tasnia hiyo zirekebishwe “sheria zinahitaji marekebisho zimetungwa muda mrefu, teknolojia imebadilika.”

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Mwinyi ameaigiza Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, kushirikiana na wadau wa habari, katika kuzifanyia marekebisho sheria hizo, hasa Sheria ya Utangazaji ya Zanzibar ya 1977 na Sheria ya Usajili wa Magazeti, zilizopitwa na muda.

Aidha, Rais Mwinyi amemuagiza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, ashirikiane na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, juu ya namna ya kuboresha mapendekezo ya Sheria inayosimamia huduma za habari.

“Na kwa bahati nzuri jambo hili limeshazungumzwa hapa, si busara kuanza kutengeneza sheria inayofafanana na wenzetu kule bara wakati ile iko katika mchakato wa kuirekebisha. Kwa hiyo ni vyema tukafanya kwa pamoja kazi hii, ili marekebisho yatakayopatikana kule sisi kwetu yawe yameingia moja kwa moja,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema “namtaka waziri fanya kazi na waziri mwenzako, katika hili la sheria basi fanyeni kazi usiku na mchana, kuhakikisha sheria hii inapatikana kwa haraka.”

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amesema Serikali yake itazifanyia mabadiliko sheria nyingine zilizo kikwazo kwa maendeleo ya visiwa hivyo na wananchi.

“Tunatambua kuwa bado zipo baadhi ya sheria ambazo huenda zikawa kikwazo cha kuyafikia matarajia yetu ya kuleta ustawi wa kiuchumi na kijamii, hivyo ni dhahidi zinahitaji kufanyiwa mabadiliko ili ziendane na muelekeo wa uchumi tunaojenga kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi yetu na Watanzania kwa ujumla,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi ameahidi kuwa, Serikali yake itaendelea kuheshimu uhuru wa habari kwani ni haki ya kikatiba na miongoni mwa sifa za msingi za demokrasia na utawala bora.

Amesema mafanikio ya Zanzibar yanahitaji mchango wa vyombo hivyo.

“Zanzibar inahitaji sana mchango wa vyombo vya habari katika kufanikisha utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya kimaendeleo, ikiwemo ujenzi wa uchumi wa kisasa unaotiliwa mkazo na matumizi ya rasilimali bahari,” amesema Rais Mwinyi.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Awali, Nape alisema atashirikiana na Mwita katika kutafuta namna ya kuzifanyia marekebisho sheria za habari zenye mapungufu.

“Ni kweli tunafanya mapitio, tumeanza mazungumzo na nikuhakikishie Rais mimi na mwenzangu tutashirikiana kuona kwamba, yale tunadhani ni mapungufu kwenye sheria yetu tuna share nao uzoefu ili tuone tunaifanya sekta ya habari iende vizuri bila mikwamo,” amesema Nape.

Nape ameahidi kuwa, mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya 2016, utakamilika kabla ya Bunge la bajeti kuanza Aprili mwaka huu.

“Ninacho waahidi kama waziri wenu, kabla ya Bunge la bajeti tutakuwa tumefikia mahali pazuri kwa marekebisho makubwa ambayo tunayakusudia. Sasa Bunge la marekebisho ya sheria likifika tutakuwa tuko tayari. Niwaahidi kwamba, ondoeni presha niko kwa ajili yenu tutafanya na mambo yatakwenda,” amesema Nape.

Kwa upande wake Mwita, amesema atashirikiana na Nape katika mchakato huo usiku na mchana, ili kuhakikisha sheria hizo zinarekebishwa.

“Tunajitahidi kuhakikisha tunawashirikisha wadau na sio tu kwenye sheria hadi sera yenyewe ili utakapotoka nayo ikipita kwenye Baraza la Wawakilishi iwe sheria ambayo imeshirikisha watu wote. Michango yote tutaifanyia kazi ili sheria itakayotoka isiwe ya kulalamikiwa bali ya kutumika,” amesema Mwita.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NMB yafadhili ziara ya mafunzo machinga, bodaboda Dar nchini Rwanda

Spread the loveBENKI ya NMB imefadhili ziara ya siku nne ya mafunzo...

ElimuHabari Mchanganyiko

Waliopata Division one St Anne Marie Academy waula, Waahidiwa kupelekwa Ngorongoro, Mikumi

Spread the love WANAFUNZI wa shule ya St Anne Marie Academy waliofanya...

Habari Mchanganyiko

Wadau wataka kasi iongezeke marekebisho sheria za habari

Spread the love  WADAU wa tasnia ya habari wametakiwa kuongeza juhudi katika...

Habari Mchanganyiko

TEF yawatuliza wadau wa habari marekebisho vifungu kandamizi

Spread the love  JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limewataka wadau wa habari...

error: Content is protected !!