WAKALA wa Barabara Tanzania (Tanroads), umekubali kutenga fedha kiasi cha Sh. 3 bilioni kwa ajili madaraja ya Halmashauri ya wilayani Masasi katika bajeti ya mwaka 2017/18, bunge lilielezwa, anaandika Dany Tibason.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi.
Bwanausi alitaka kujua ni lini madaraja ya Shaurimoyo, Nakalolo na Miesi yatajengwa ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa na adha kubwa ya usafiri.
Akijibu swali hilo, Jafo amesema kutokana na ufinyu wa bajeti ya Halmashauri hiyo, Wakala huo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imekubali kutenga fedha hizo kwa ajili ya ujenzi ambao utaanza mara moja baada ya fedha kupatikana.
Amesema Halmashauri hiyo kwa msaada wa Tanroads imekamilisha usanifu wa madaraja yanayohitajika kujengwa katika mito ya Mpindimbi-Shaurimoyo na Kanyimbi-Nakololo ambayo kwa pamoja yatagharimu Sh. 3 bilioni.
Jafo akijibu swali hilo alisema tathmini imeshafanyika tayari na ujenzi utaanza baada ya Bajeti hiyo kupitishwa.
Leave a comment