October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tanroads, Polisi wapewa rungu kudhibitini uhalifu Kimara, Kibaha

Barabara ya Morogoro

Spread the love

 

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi nchini Tanzania, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameitaka Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), mkoa wa Dar es Salaam kuzungumza na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na watu wanaotekeleza uhalifu katika barabara ya njia nane ya Kimara hadi Kibaha. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, Kasekenya amesema amekerwa na kitendo cha wananchi kutotumia vivuko vilivyowekwa kwa ajili ya kuvuka barabara hiyo ya njia nane eneo la Stendi ya Magufuli, Mbezi.

Naibu Waziri huyo amesema hayo leo Jumatatu, tarehe 3 Januari 2022, wakati akifanya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19 iliyojengwa kwa fedha za ndani zaidi ya Sh.218 bilioni.

Amesema, taarifa alizonazo zinaonesha kuwepo vitendo vya baadhi ya watu kufanya uhalifu kwa kuweka mapipa na mawe kuzuia magari na kuwaibia wananchi jambo ambalo linaenda kinyume na kusudio la ujenzi wake.

“Nimepata taarifa kuna wenzetu wanatumia fursa ya ujenzi unaoendelea, kwa kutenda uhalifu, naomba Tanroads ishirikiane na vyombo vua usalama kudhibiti vitendo hivyo,” amesema.

Mhandisi Kasekenya amewataka Tanroads kuangalia uwezekano wa kuondoa vizuizi hivyo iwapo havina kazi kwa sasa ili kukabiliana na matukio hayo ambayo yanahatarisha maisha ya watumiaji wa barabara.

Kwa upande mwingine, Kasekenya amewaomba wananchi kutumia vivuko vilivyoanishwa katika barabara hiyo ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea.

Pia, aliwataka wananchi kutotupa taka ngumu katika barabara na mifereji ili kuhakikisha usalama wa barabara unakuwa endelevu.

Halikadhalika, Kasekenya amewataka madereva wa magari makubwa kuhakikisha wanapima magari yao kuanzia bandarini ili kuepuka kubebea mizigo inayochangia uharibifu wa barabara.

Kwa upande mwingine Naibu Waziri Kasekenya ameitaka Tanroads Dar es Salaam, kuhakikisha mradi wa ujenzi wa barabara na madaraja unakamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu kama makubaliano ya mkataba yanavyotaka.

Naibu waziri ameitaka Tanroads kusimamia kwa karibu ujenzi wa barabara na madaraja yaliyopo katika mradi huu, ili ubora unatakiwa upatikane.

Aidha, Kasekenya alisema Wizara ya Ujenzi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) watahakikisha barabara za jiji hilo zinajengwa kwa kasi.

Akizungumzia Mradi huo Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Harun Senguku alisema, mradi huo wa njia nane umeongezeka muda wa utekelezaji baada ya kuongezwa maeneo ya ujenzi.

“Kwa ujumla mradi huu ulikuwa umekwisha katika awamu ya kwanza ambayo ilihusu njia nane, madaraja na mifereji na barabara za kuunga, lakini Serikali imeongeza ujenzi wa madaraja katika eneo la Kwa Yusuph na Stendi ya Magufuli, hivyo matarajio ni ikifika Juni 2022 itakuwa imekamilika,” amesema.

Mhandisi Senguku amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kuondoa foleni, hali ambayo itaongeza uzalishaji na kukuza uchumi.

Amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 77 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 218 zikiwa fedha za ndani.

error: Content is protected !!