Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Tangulia Profesa Honest Ngowi, utakumbukwa daima
Makala & Uchambuzi

Tangulia Profesa Honest Ngowi, utakumbukwa daima

Spread the love

NILIPATA mshtuko mkubwa kupokea taarifa mbaya ya kifo cha Profesa Honest Ngowi kilichotokana na ajali ya gari kutoka kwa mwanachama mwenzetu wa kundi sogozi la ‘Wanazuoni’, Onesmo Ole Ngurumwa ambaye ni Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu.

Taarifa ya kifo hicho ilithibitishwa baadaye na Idara ya Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa Idara ya Mawasiliano Mzumbe, Profesa Ngowi alikuwa njiani kwenda Kampasi kuu mkoani humo kikazi na ikawaomba wafanyakazi na Menejimenti wawe watulivu.

Kifo cha mchumi huyo kilitokea eneo la Mlandizi mkoani Pwani baada ya gari alilokuwa anatumia kusafiri kuangukiwa na kontena la Lori la mizigo katika barabara ya Morogoro. Ni jambo kusikitisha sana namna kifo chake kilivyotokea.

Wakati wote nilipokuwa napokea taarifa hiyo mikono yangu ilitetemeka, nilistaajabu namna kifo chenyewe kilivyotokea, yaani mazingira ya kifo chake yanaudhi pakubwa, na kuzua maswali ni namna gani Makontena hayo yanachomoka kwenye magari? Hayafungwi kama inavyotakiwa? Nawauliza wataalamu wa usafairishaji. Nawauliza ili kuibua mjadala juu ya matukio hayo.

Binafsi, nimekumbuka mengi kuhusiana na gwiji huyo wa uchumi. Nilikuwa msomaji wa maandiko ya Profesa Ngowi miaka mingi iliyopita wakati akiandikia gazeti la Rai Nguvu ya Hoja lililomilikiwa na kampuni ya New Habari(2006) Corporation na kuchapishwa mara moja kwa wiki (kila Alhamis). Aliyekuwa mhariri wangu wa makala Deus Ngowi ndiye aliyenifanya nikamfahamu Profesa Ngowi.

Kila mara nilipata nafasi ya kuzisoma makala hizo kwenye safu ya uchumi iliyokuwa inaruka hewani. Na kwa vile Deus Ngowi ni mmoja wa wahariri walionipika basi ikawa rahisi kufahamu mengi kuhusu mwanazuoni huyo na kunufaika na maarifa yake.

Kwa kipindi hicho nilimwelewa kama mchambuzi wa masuala ya uchumi ambaye alidadavua katika mada tofauti hadi pale nilipokuja kukutana naye kwenye shughuli za uandishi wa habari. Pia katika uandishi wake ameonesha wazi mapenzi yake kwa sekta binafsi, na alitambua kuwa ni mhimili wa maendeleo ya nchi kuliko kutegemea njia za serikali peke yake.

Jambo zuri zaidi ni pale Dk Richard Mbunda alisaidia niwe karibu na Profesa Ngowi kuliko awali kwa kunijumuisha kwenye kundi sogozi la Wanazuoni ambalo hutumika kuendesha mijadala ya aina mbalimbali kuanzia uchumi,jamii,michezo,burudani pamoja na utani wa hapa na pale.

Ngowi hakujali kiwango cha elimu ya mtu. Daima alipenda kujifunza, na ndio maana alituasa kuishi vizuri na watu. Tukio lililomfanya kukumbusha nasaha hizo ni pale alipohudhuria mafunzo fulani na kukutana na wakufunzi ambao ni wanafunzi wake wa zamani. Wanafunzi hao walishtushwa walipoona mwalimu wao wa zamani ni miongoni mwa wanafunzi wanaotakiwa kufunzwa, na hapo ndipo Ngowi alisisitiza kuishi vizuri na watu na maisha ni mzunguko.

Katika maisha ya kundi sogozi na Profesa Ngowi yalikuwa yale ya kaka na wadogo, baba na watoto, mwalimu na wanafunzi,kiongozi na wananchi,uungwana na ustaarabu,utani mwingi,ucheshi na hamasa, vitu ambavyo vilikuwa sehemu ya maisha yake.

Aidha, katika tukio lingine ni pale alipokuwa anahitaji kuona mwanae anatimiza ndoto ya kuwa rubani. Alihakikisha anapatiwa kila aina ya msaada, aliomba mawasiliano na kuunganishwa na wadau mbalimbali kupitia kundini mwetu.

Alitueleza matamanio ya binti yake kuwa rubani,masomo na aliomba ushauri pia ili aweze kumsaidia zaidi binti huyo. Humo alishauriwa aina ya vyuo na namna ya kufanikisha azma ya kumsaidia mtoto wake kuwa rubani.

Tukio moja ninalokumbuka ni pale alipohitaji binti yake asimame kwenye majukwaa kutoa ushuhuda kuwa hata mtoto wa kike anaweza kutimiza malengo na ndoto zake ikiwa atasimamiwa vizuri. Tukio hilo la kutaka binti yake awe miongoni mwa watoa ushuhuda kwenye kongamano moja la wanawake lililofanyika Mlimani City jijini Dar es salaam hivi karibuni.

Prof. Ngowe akiwa na dereva wake Innocent enzi za uhai wao

Jitihada alizofanya kupitia kwetu kuwapata waandaaji hadi kufanikiwa ni ishara tosha kuwa alikuwa tayari kutengeneza alama katika maisha ya binti yake na nchi yake kuhakikisha binti yake anakuwa rubani mwenye kuhamasisha wengine.

Aghalabu alikuwa aakituambia kuwa wenye watoto wa kike wasiwasahau mazingira magumu ya kutimiza ndoto zao, bali wawe daraja la mazingira ya kuja wataalamu wente tija kwa taifa.

Aidha, alikuwa anasisitiza ni muhimu watoto wa kike waungwe mkono na kusaidiwa kutimiza malengo zao bila ubaguzi. Kwake mtoto ni yeyote bila kujali jinsia, na aliamini uwezo wao ni sawa.

Ngowi alikuwa mwanachama ambaye hakujali tofauti za itikadi wala umri, kwake yeye uhusiano wa watu ulijengwa katika uungwana na ustaarabu. Hakuona aibu kuomba mchango wa mawazo kutoka hata watu aliowazidi elimu,maarifa,uzoefu na hadhi.

Hakuona aibu kuwasilisha mada yake ambaye angependa ashauriwe vitu au mambo ya kuzungumziwa. Hakuwa mchoyo wa kuwasilisha maandiko yake na tafiti kadhaa alizowahi kufanya kwa nyakati tofauti.

Amekuwa gumzo kwa mada mbalimbali kupitia vituo vya Televisheni na redio, hata kwenye makundu sogozi alikuwa akishiriki mijadala, na hakuwa mchoyo wa maarifa.

Hadi ameaga dunia Profesa Ngowi alikuwa Mkuu wa chuo cha Mzumbe Kampasi ya Dar es salaam, akiwa amebobea katika uchumi na mwanachama wa Jumuiya ya wachumi Tanzania.

Ama hakika taifa letu limepoteza nguli wa uchumi ambaye ameniachia swali, imekuwa Kontena hizo zikawa chanzo cha kukatisha maisha yake? kwamba si uamuzi wa Mwenyezi Mungu bali shughuli za binadamu ndizo zimekatisha uhai wake. Tutateketea hadi lini?

Tangulia Ngowi, safari yetu ni moja, nasi tutakufuata huko.

Ndimi mwanachama mwenzio wa Wanazuoni.

Makala haya yameandaliwa na Markus Mpangala – mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisasa nchini Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!