October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tanesco yapanguliwa, January ateua vigogo

Nehemia Mchechu

Spread the love

 

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limeendelea kusukwa upya baada ya Waziri wa Nishati, January Makamba kuteua vigogo kuwa wajumbe wa bodi ya shirika hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

January amefanya uteuzi huo jana Jumamosi, tarehe 25 Septemba 2021, ikiwa ni saa chache kupita tangu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuteua viongozi wapya wa shirikahilo.

Rais Samia alimteua Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco kuchukua nafasi ya Dk. Alexander Kyaruzi
Kabla ya uteuzi huo, Issa alikuwa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji na Usimamizi wa Miradi (PDB) iliyosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Mara baada ya Rais Samia kufanya uteuzi huo, Waziri January akatangaza majina ya wajumbe nane wa bodi hiyo ambao; ni aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu na Zawadia Nanyaro.

Wengine ni, aliyewahi kuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Masawe, Balozi Mwanaidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim, Christopher Gachuma na Abubakar Bakhresa, mtoto wa mfanyabiashara mkubwa nchini Tanzania, Said Salim Bakhresa.

Abubakar Bakhresa

Bodi hiyo mpya inachukua nafasi ya bodi iliyokuwepo ambayoiliteuliwa tarehe 13 Novemba 2019 na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk. Madard Kalemani ambaye nafasi yake imechukuliwa na January Makamba.

Wakati Dk. Kalemani anaiteua bodi hiyo alisema watakaa madarakani kuanzia 13 Novemba 2019 hadi 12 Novemba 2022.

Waliokuwa wajumbe wa bodi hiyoni, Balozi Dk James Nzagi, Dk. John Kihamba (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saam – DUCE) na Dk Lugano Wilson (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi na Mkuu wa Teknolojia za Nishati – TIRDO).

Pia, alikuwemo John Kulwa (Mkuu wa Idara ya Ukaguzi Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi – MUHAS) na Denis Munumbu (Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru).

Katika panga, pangua hiyo ndani ya Tanesco, Rais Samia alimteua Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu. Kabla ya uteuzi huo, Chande alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika ambaye amechukua nafasi ya Dk. Tito Mwinuka.

Dk. Mwinuka aliteuliwa tarehe 01 Januari 2017 na aliyekuwa Rais, Hayati John Pombe Magufuli kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Tanesco kuchukua nafasi ya Mhandisi Felchesmi Mramba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Baadaye Dk. Mwinuka alithibitshwa kuwa mkurugenzi mkuu.

Waziri Nishati, January Makamba

Dk. Mwinuka wakati anateuliwa alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, katika uteuzi alioufanya Rais Samia, amemrejesha kundini Mhandisi Felschemi Mramba kwa kumteua kuwa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu.

Kabla ya uteuzi huo, Mramba alikuwa Mshauri Mkuu wa Kiufundi (Chief Technical Advisor) – Tanesco training School

Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga alitangaza kuwahamisha watumishi Waandamizi watano toka Tanesco kwenda Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine.

Watumishi hao ni, Mhandisi Khalid James (Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji), Mhandisi Raymond Seya (Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Masoko) na Mhandisi Isaac Chanje (Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji).

Pia yumo, Nyelu Mwamaja (Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi) na Amos Ndegi – (Mwanasheria wa Tanesco).

error: Content is protected !!