Monday , 27 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Tamwa yatoa mbinu mtoto wa kike anavyoweza kufikia ndoto zake
Habari Mchanganyiko

Tamwa yatoa mbinu mtoto wa kike anavyoweza kufikia ndoto zake

Spread the love

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimewataka watoto kuvunja ukimya na kupaza sauti mara tu waonapo dalili za kufanyiwa ukatili ili kuwawezesha kufikia ndoto zao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Pia, kimeitaka jamii kuacha mifumo yote inayomkandamiza mtoto wa kike badala yake kuwepo usawa na ulinzi kwa watoto wa jinsia zote.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe kupitia tamko alilolitoa leo Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020 ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Duniani.

Kila mwaka 11 Oktoba dunia huadhimisha siku hii ili kukumbushana madhila wanayopitia watoto wa kike na kuikumbusha jamii nguvu iliyomo kwa watoto hao ambapo kauli mbiu inasema: Sauti yangu, ni mustakabali wetu wa usawa.’

Joyce amesema, kupitia miradi mbalimbali waliyoifanya Tamwa, imebaini kuwepo mifumo kandamizi kwa watoto wa kike.

Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe

Amesema, mifumo hiyo imesababisha baadhi ya jamii kukumbatia vitendo vya  ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni, manyanyaso kutoka ndani ya familia, kunyimwa haki ya kupata elimu na kugubikwa na mzigo wa majukumu ya kazi za nyumbani.

Amesema, changamoto hizi na nyingine nyingi, zimechangia mtoto wa kike kukosa fursa ya elimu, kuathirika na maradhi, kuathirika kisaikolojia na kukosa nafasi yake ya kufurahia utoto wao kutokana na mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

“Taifa lenye amani ni lile linalothamini haki za watoto, ikiwamo haki ya kuishi kwa furaha, kupata huduma za msingi ikiwemo huduma ya afya, elimu na amani,” amesema Joyce.

Amesema, kwa mujibu wa takwimu za madawati ya jinsia nchini Tanzania, imebainika mimba za utotoni ziliongezeka kwa kasi wakati wa likizo ya miezi mitatu  mwaka huu iliyosababishwa na mlipuko wa virusi vya corona.

Kutokana na kadhia hiyo, Joyce amesema, Tamwa inaiomba serikali kuandaa utaratibu wa ulinzi, utoaji taarifa na ufuatiliaji kwa watoto hasa wakati wa dharura za milipuko ya magonjwa au majanga kama Covid-19 ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika.

Amesema, takwimu za uhalifu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) zinaonyesha, katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2016 jumla ya kesi 10,551 za uhalifu dhidi ya watoto ziliripotiwa vituo vya polisi, ukilinganisha na kesi 9,541 kuanzia Januari hadi Desemba 2015.

“Uhalifu huo ni pamoja na ubakaji, utelekezaji wa watoto, wizi wa watoto, ukeketaji na mashambulio ya kudhuru mwili.”

“TAMWA tunaomba wazazi, walezi na watoto wa kike,wanaofanyiwa ukatili, wavunje ukimya, kwani zipo asasi, taasisi na vyombo vya serikali ambavyo wanaweza kuvitumia kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia,” amesema Joyce.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben

Mwenyekiti huyo amesema, ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto(UNICEF) inaeleza watoto wa kike milioni 12 huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 kila mwaka.

Amesema, watoto wa kike takribani milioni 6 hadi 17 duniani kote hawajapata nafasi ya kwenda shule na inaelezwa kuwa watoto wa kike milioni 15 duniani, wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19 wameathirika kisaikolojia kutokana na manyanyaso ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo kubakwa, vipigo na udhalilishaji wa kingono.

“Takwimu zinazojitokeza zinaonyesha kuwa tangu kuzuka kwa COVID-19, unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana (VAWG), na hasa unyanyasaji wa nyumbani, umeongezeka kwa kasi,” ameaema Joyce.

Amesema,” Tukumbuke watoto hawa, wakiwamo wa kike ni taifa la kesho, hivyo basi wanapoharibiwa misingi bora ya maisha, tunakwenda kuharibu mustakabali wa kesho ambapo hatuwezi kupata wafanyabishara, wakulima, mawaziri, wabunge, wakurugenzi na viongozi bora wanawake, iwapo watoto wa kike wa sasa  watabakwa, watapata mimba, wataozwa katika umri mdogo, watashambuliwa na kunyanyaswa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoMichezo

NBC yakabidhi Kombe la Ubingwa wa  Ligi Kuu ya NBC, yaahidi maboresha zaidi

Spread the loveMdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC (NBC Premiere League),...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kasekenya aipa Tanroads wiki kukarabati barabara Morogoro

Spread the loveNaibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ametoa wiki moja...

ElimuHabari Mchanganyiko

Rubani mtarajiwa Tusiime awashangaza wazazi

Spread the loveWAZAZI walioshiriki siku ya taaluma na maonyesho ya shule ya...

Habari Mchanganyiko

Wanne wadakwa kwa kusafirisha punda 46 nje ya nchi

Spread the loveJeshi la Polisi kikosi cha kupambana na kuzuia wizi wa...

error: Content is protected !!