Thursday , 25 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Tamwa yajitosa rushwa ngono vyombo vya habari
Habari Mchanganyiko

Tamwa yajitosa rushwa ngono vyombo vya habari

Spread the love

CHAMA cha Wanahabri Wanawake Tanzania (Tamwa) kimezindua mradi wa ‘rushwa ya ngono miongoni wanahabari wanawake katika vyombo vya habari’ kwa kuangalia tatizo hilo na jinsi ya kulimaliza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Septemba 2020 jijini Dar es Salaam kwa kukutana na waandishi wa habari wenyewe, wahariri, wamiliki na wadau wengine wa habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa tarehe 2 Oktoba 2020 jijini Dar es Salaam amesema, waandishi ni kundi muhimu ambalo likishaelimika litaweza kupambana na tatizo hili kwa kuwaelimisha wengine.

“Wanahabari wameonekana kuwa kimya kuhusu matukio hayo, aidha kwa kuogopa kupoteza ajira zao au pengine wakichelea kuaibika zaidi pindi watakapoweka wazi masaibu yao.”

“Kimsingi, rushwa ya ngono haikubaliki na ni tabia isiyopendeza inayoshusha utu na kuwafanya waathirika kudhalilika, kupata msongo wa mawazo na kukosa kujiamini mahala pa kazi, lakini baya zaidi ni matukio mengine hayaripotiwi,” amesema Rose

Rose amesema baadhi ya watafiti kama Barton A na Storn (2014) walibaini asilimia 48 ya wanahabari wanawake waliohojiwa walikiri wamewahi kukumbana na rushwa ya ngono ndani ta vyumba vya habari kwa namna moja au nyingine na asilimia 83 kati yao walisema hawakuripoti matukio hayo.

“Ombwe hili ni kubwa na huenda likawaathiri hata wanahabari wachanga walio vyuoni, ambao huenda wakakataa kuingia katika tasnia hii na hivyo kuizorotesha tasnia lakini baya zaidi, kukosa wanahabari wanawake katika nafasi za juu za uongozi na wenye mafanikio katika tasnia hiyo,” amesema Rose.

Mkurugenzi huyo amesema, imebainika vyombo vingi vya habari nchini havina sera madhubuti zilizowekwa kuwaongoza wanahabri katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinapowakumba ikiwemo masuala ya rushwa ya ngono katika mazingira ya kazi hivyo kuchangia kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono.

“Hivyo basi, kukiwa na ombwe kama hilo, Tamwa katika utekelezaji wa mradi huu, itafanya tathimini kwa kupitia maswali, ili kujua yanayowasibu wanahabari,” amesema

Amesema, baada ya kufanya tathimini, Tamwa itawajengea uwezo wanahabari, wakiwemo wahariri na wanawake wanahabari walio katika vyombo vya habari kisha Tamwa itashirikiana na vyombo vya habari kufanya uchechemuzi.

Kufanya mazungumzo na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuwashirikisha matokeo ya tathimini na kuelimisha jamii kuhusu rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari na kutumia mitandao ya kijamii.

Rose amesema, Tamwa itashirikisha na wadau mbalimbali wa habari wakiwemo, Taasisi ya vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa-Tan), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (Osha).

Amesema, mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ni kitovu cha vyombo vya habari nchini zikiwemo redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.

“Tamwa inaamini kufanya tathimini ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na kuwajengea uwezo wanahabari, itawezesha pia kufahamu na kuandika vyema habari zinazohusu rushwa hii ambayo kwa mujibu wa mila na desturi za Watanzania walio wengi imekuwa ikizungumzwa kwa kificho au kutozungumzwa kabisa,” amesema.

Rose amesema “tunataka wanahabari wapaze sauti zao, tuvunje ukimya, wayazungumze yanayowasibu na kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia wa aina hii ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari ikiwa ni pamoja na kuua vipaji.”

“Pasipo kuvunja ukimya uliotanda dhidi ya suala la rushwa ya ngono, waathirika kujengewa uwezo wa kukusanya vidhibiti visivyokuwa na mashaka yoyote, taasisi yenye mamlaka ya kushughulikia makosa haya haziwezi kufanya kazi yake kwa ufasaha na kuleta mabadiliko katika jamii yetu,” amesema

Naye Brian Mshana, Afisa Mwandamizi Idara ya Ufuatiliaji na Uwezedhaji wa WFT amesema, mradi huo ni wa kimkakati wa kuangalia mazingira wanayokutana nayo wanahabari wa kiume na kike na jinsi ya kushughulikia.

“Wanawake, wasichana na wote tunapaswa kufurahia maisha yetu lakini kumekuwa na ukatili mkubwa wa kingono na sisi tunataka kuvunja ukimya. Siyo kutafuta mchawi bali kuangalia tatizo na jinsi ya kulimaliza,” amesema

Mshana amesema “kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kwa wale wote watakaokuwa wakibainika kuhusika na Takukuru watakuwa na hamu ya kusubiri huu mradi.”

“Matokeo ya mradi huu yatakuja na matokeo chanya. Rushwa ya ngono inaua na inadhalilisha,” amesema

Kwa upande wake, Neema Kasambuliro, Afisa Habari na Utafiti wa Misa-Tan amesema, mradi huo utakuwa chachu ya kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari.

“Uhuru wa kufanya kazi kwa kila mwandishi awe wa kiume, awe wa kike pasina kuoneana kwa jinsia yake au nini,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

THRDC yaongeza mkataba wa ushirikiano na ABA

Spread the love  MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),...

Habari Mchanganyiko

Rufaa ya Equity Benki, State Oil yakwama

Spread the loveMAHAKAMA ya Rufani, jijini Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea na...

Habari Mchanganyiko

Bodaboda waeleza mafanikio mafunzo usalama barabarani

Spread the loveMADEREVA bodaboda katika Jiji la Dodoma wameeleza jinsi mafunzo ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yaahidi kuendelea kuunga mkono Serikali za Mitaa

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya...

error: Content is protected !!