April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TAMISEMI yaja na sharti jipya kwa vyama vilivyojitoa

Mwita Waitara, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI

Spread the love

WIZARA ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI imewataka wagombea wa vyama vya upinzani, vilivyojitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kuandika barua za kujitoa katika uchaguzi huo, kabla ya saa 10:00 jioni ya leo tarehe 16 Novemba 2019. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Sharti hilo amelitoa Mwita Waitara, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wakati akizungumza  na mtandao wa MwanaHALISI ONLINE, kwa njia ya simu.

Waitara amefafanua kuwa, wagombea wanaotakiwa kuandika barua za kujitoa, ni wale walioteuliwa kugombea katika uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019.

Waitara amesisitiza kuwa, muda huo ukifika pasipo wagombea husika kuandika barua ya kujitoa, wizara yake itaendelea kuwatambua, na kuwa watapigiwa kura, hata kama vyama vyao vimetangaza kujitoa.

“Sisi hatupokei barua ya chama ya kujitoa, tunapokea barua kutoka kwa mgombea mwenyewe. Hata kama chama kimejiondoa lakini mgombea akaendelea kushiriki, atashiriki sababu kanuni zinaruhusu.

Kila mgombea anayetaka kujitoa mwisho wa kuandika barua, ni leo saa kumi ikizidi hapo, kama kuna mgombea aliyeteuliwa na msimamizi wa uchaguzi, ataendelea kwenye mchakato na atapigiwa kura,” amesema Waitara.

Aidha, Waitara amesema kuna baadhi ya wagombea wa vyama vilivyojitoa hasa kwenye maeneo ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na Tarime mkoani Mara, wamegoma kujitoa katika uchaguzi huo.

“Kuna baadhi ya maeneo wagombea wao wamegoma kujitoa, na uchaguzi siyo chama, uchaguzi ni mgombea. Anayejitoa sio chama, mwanachama ndiyo anajitoa, mambo ya chama ni ya kwao, sisi tutaendelea kuwatambua,” amesema Waitara.

Hadi sasa vyama takribani nane, ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi  na Chama cha Ukombozi wa Umma, vimetangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo, baada ya wagombea wake wengi kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi.

error: Content is protected !!