November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watu 11,000 kutajirika Jangwani – Dar

Spread the love

JUMLA ya watu 11,000 waliopo katika kaya 3,800 wakiwamo wapangaji wanatarajiwa kulipwa fidia kuanzia mwaka 2023 kupisha uboreshaji wa Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unaratibiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) kupitia Mradi wa uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia (WB) chini ya TARURA na DMDP, Humphrey Kanyenye akizunguma na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati itakayotekelezwa katika uboreshaji wa eneo la Bonde la Msimbazi ikiwa ujenzi wa daraja la Jangwani unaotarajiwa kuanza Aprili mwaka 2023.

Aidha, ujenzi wa daraja la Jangwani utakaoratibiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), pia utaanza Aprili mwaka 2023. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Hatua hiyo inakuja baada ya Novemba 21, 2022 Serikali kusaini mkataba na Benki ya Dunia inayotoa mkopo wa riba nafuu dola za Marekani milioni 535 sawa na trilioni Sh1.2 ambazo kati yake dola milioni 260 (bilioni 463.98) kwa ajili ya mradi wa bonde hilo la Msimbazi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 24 Novemba, 2022 jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia (WB) chini ya TARURA na DMDP, Humphrey Kanyenye ametaja mikakati itakayotekelezwa.

Amesema jukumu la kwanza litakaloanza kutekelezwa ni kurejesha uoto wa asili katika eneo la Pugu kwa kupanda miti hasa ikizingatiwa bonde la Msimbazi limeanzia katika eneo hilo ambalo limeharibiwa pakubwa kutokana na ukataji wa miti hovyo.

“Bonde limegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ni kule Pugu, katikati ni hapa Tabata na Segerea na ya tatu ni Kigogo,” amesema.

Mkakati wa pili ni kujenga kingo za mto na madaraja yaliyokatika ambapo sasa yatajengwa upya.

Mkakati wa tatu ni kujenga mabeseni maalumu ambayo yatapunguza kasi ya maji lakini yatatumika kama mtego wa mchanga ndani ya mto huo hasa ikizingatiwa mchanga huo unafaa kwa matumizi.

“Pia tutajenga mabwawa ya zaidi ya matatu kwa ajili ya kutunzia maji. Bwawa la aina hii limejengwa Chuo cha maji Dar es Salaam na sasa eneo la Sinza hakuna tena mafuriko.,” amesema.

Mkakati wa nne amesema ni ujenzi wa daraja la Jangwa ambalo litakuwa na urefu wa mita 390, kutanua mto huo hadi kufikia upana wa mita 60 na kutengeneza matuta yenye urefi wa mita 30 kando ya mto huo.

Amesema maboresho ya mto huo ambao unapokea maji pia kutoka katika mito midogo ikiwamo Kibangu na mto Ng’ombe, yatawezesha upatikanaji wa hekta 57 ambazo zitakabidhiwa kwa kampuni zinazojihusisha na biashara za Real Estate.

“Baada ya uboreshaji katika eneo la Jangwani pekee, kutapatikana jumla ya hekta 420 zitakazotumiwa kwa uwekezaji ikiwamo maduka makubwa ya kibiashara, viwanja vya michezo na ofisi za Serikali,” Mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia (WB) chini ya TARURA na DMDP, Humphrey Kanyenye ametaja mikakati itakayotekelezwa.

“Uwekezaji huo tuna uhakika utarejesha fedha za mkopo huo wa Benki ya Dunia ndani ya kipindi kifupi,” amesema.

Amesema katika eneo hilo ambalo sasa kuna Ofisi za mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) pamoja na maegesho ya magari ‘depo’, itahamishiwa katika eneo la Ubungo maziwa.

Pamoja na mambo mengine katika fidia hiyo ya wakazi wa eneo hilo la Jangwani, pia wapangaji kuna kiwango cha fedha watakachopatiwa ili kuwawezesha kwenda kupanga eneo lingine, wakati waliokuwa wamejenga nyumba 3,291 katika eneo hilo watapatiwa fedha kwa ajili ya kwenda kununua viwanja na kujenga maeneo mengine.

Amesema kabla na baada ya fidia hiyo watapewa mafunzo maalumu yatakayowasaidia kutumia fedha hizo vizuri kwani lengo la mradi huo ni kutomsababisha aliyekuwa mkazi wa eneo hilo kukumbwa na umaskini.

error: Content is protected !!