July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tamasha la Nyerere kujadili migogoro ya ardhi

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Spread the love

TAMASHA la saba la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kupaza sauti za wanyonge linatarajiwa kufanyika 13 -15 Aprili, mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Tamasha hilo litafanyika katika ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi.

Mada kuu ya mwaka huu ni “Ubinafsishaji wa Haki za Kijamii kwa Wanyonge”.

Akizungumza na MwanaHALISIOnline leo, Prof. Penina Mlama – Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere – waandaaji wa tamasha hilo, amesema mada hiyo inalenga kuangalia “namna ubinafsishaji katika masuala ya ardhi na madini unavyowaathiri wananchi wa tabaka la chini”.

“Wazungumzaji kutoka katika vijiji watapewa fursa ya kupaza sauti na kusimulia athari wanazokumbana nazo kwenye maeneo yao. Hawa ndio waathirika namba moja wa utekelezaji wa sera za ubinafsishaji na mfumo wa kibepari,” amesema Prof. Mlama.

Prof. Mlama amesema, Kigoda kimewaalika wawakilishi kutoka; Tanzania ambao watazungumzia athari za mgogoro wa ardhi kwenye shamba la mpunga la Kapunga lililopo wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya; mgogoro wa ardhi Loliondo, Arusha; mgogoro wa wafugaji na wakulima Kilosa mkoni Morogoro na mgogoro wa madini Geita.

“Pia tutakuwa na wazungumzaji kutoka Garissa Kenya ambao watazungumzia mgogoro wa ardhi; Wazungumzaji kutoka Mubende na Karamoja Uganda ambao pia watazungumzia migogoro wa ardhi katika vijiji vyao,” amesema Prof. Mlama.

Aidha, amesema watakuwepo wazungumzaji kutoka nchini Afrika Kusini ambao watazungumzia uchimbaji wa madini ya Platinum ambao umeibua ugomvi kati ya wanakijiji na wawekezaji.

Waalikwa wengine ni maprofesa, wanaharakati na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

“Kazi kubwa ya Kigoda cha Mwalimu ni kudumisha fikra za Mwl. Nyerere, ambazo zililenga kupigania wananchi masikini, ambao kwa sasa wanaonekana kushidwa kupambana na mifumo ya kinyonyaji,”amesisitiza Mlama.

error: Content is protected !!