SIKU chache baada ya wanamgambo wa Taliban kuipindu Serikali ya Afghanistan, wanajeshi hao wameanza kusaka mahasimu wao. Anaripoti Noela Shila, TUDARCo, kwa msaada wa mitandao ya kimataifa … (endelea).
Taliban waliipindua Serikali hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ashraf Ghani, Jumapili ya tarehe 15 Agosti 2021, baada ya kuiteka Ikulu ya Afghanstan pamoja na miji muhimu 23 kati ya 34 nchini humo.
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC, wanamgambo hao baada ya kufanya mapinduzi hayo, wameanza kufanya msako wa nyumba kwa nyumba, kuwatafuta wapinzani wao ikiwemo watu waliofanya kazi na Jumuiya ya Kujihami (NATO) na Serikali ya Afghanistan, katika kuwaondoa madarakani mwaka 2001.
Taarifa ya msako huo imetolewa na Umoja wa Mataifa (UN), ukisema kwamba, Taliban wameanza kuingia nyumba kwa nyumba, kuwatafuta wapinzani wao, huku wakizitishia familia zao.
Christian Nellemann, aliyeandaa ripoti ya UN kuhusu matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, unaofanywa na Taliban, amesema maisha ya watu wanaolengwa na wanamgambo hao, yako hatarini.
Kundi la wanamgambo hao wenye itikadi kali ya kiislamu, liliiongoza Afghanistan kuanzia 1996 hadi 2001, ambapo liling’olewa na majeshi ya mataifa ya kigeni ikiwamo Marekani.
Leave a comment