August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TAKUKURU yamnasa askari ‘feki’ wa JWTZ

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, imemtia nguvuni Felister Mawe kwa tuhuma za kujifanya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huku akiomba rushwa, anaandika Moses Mseti.

Ernest Makale, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, ametoa taarifa hiyo leo asubuhi alipozungumza na wanahabari ambapo ameeleza kuwa, Mawe alikamatwa baada ya kuomba rushwa ya Sh. 500, 0000/=

“Mtu huyo anayejifanya askari wa JWTZ alikamatwa 10, Oktoba mwaka huu, akiwa katika hoteli ya Wendele iliyopo Kirumba, Mwanza. Mtuhumiwa huyu amekuwa akisaidiwa utapeli huu na Sophia Chacha ambaye ni mwanajeshi mstaafu,” amesema Makale.

Kabla ya mtuhumiwa huyo kukamatwa,  alikuwa ameomba kiasi cha Sh. 500,000/= ili amsaidie mwananchi mmoja kujiunga na JWTZ na tayari alikuwa amepokea kiasi cha Sh. 24,000/= kutoka kwa mwananchi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.

Hata hivyo Makale amesema kuwa, mtuhumiwa huyo amekuwa akiomba na kupokea kiasi cha Sh. 500,000/= kutoka kwa watu mbalimbali wanaohitaji kujiunga na jeshi hilo kwa ahadi kuwa atawasaidia kupata nafasi hizo.

Katika tukio linguine, Takukuru wilayani Misungwi jijini hapa imemfikisha mahakamani Steven Kushoka, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSD), kwa tuhuma za kupokea Sh. 400,000/= ili asimchukulie hatua za kinidhamu mwalimu Kitoki Mgaya.

Mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kutenda kosa hilo tarehe 16 Januari, mwaka huu ambapo alipokea Sh. 300,000 na kisha baadaye tarehe 27 Aprili, mwaka huu alipokea tena Sh. 100,000/= kupitia miamala ya M pesa, kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Kesi hiyo Imefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Misungwi mbele ya Hakimu Ruth Mkisi na Mwema Mella, mwendesha mashtaka wa Takukuru.

error: Content is protected !!