May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Takukuru yaitunuku tuzo MwanaHALISI TV

Spread the love

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imeitunuku tuzo Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), kwa kutambua mchango katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea)

HHPL inayozalisha MwanaHALISI TV na MwanaHALISI Online, imepewa tuzo hiyo jana Alhamisi tarehe 28 Januari 2021, ikiwa ni miongoni mwa vyombo vya habari nchini Tanzania, vilivyopewa tuzo hizo na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo.

Mbungo alisema, vyombo vya habari, vina mchango mkubwa katika mapambano ya rushwa kwa kuelimisha na kuhabarisha jamii “na sisi Takukuru, bila vyombo vya habari, hatuwezi kufanikiwa kwani kalamu ina nguvu zaidi.”

“Tunawaomba waandishi wa habari, kutumia vyema kalamu zenu katika kuhabarisha, kuhamasisha wananchi kuepuka na kuachana na rushwa.”

“Kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari kwenye mapambano haya, tunawatunuku vyeti kama mchango wenu kwenye mapambanbo haya,” alisema Mbungo kwenye hafla hiyo iliyoambana na uzinduzi wa Televisheni mtandaoni ya Takukuru ‘Takukuru TV.’

Pia, HHPL ni wazalishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, Mseto na Mawio.

Baadhi ya vyombo vingine vilivyotunukiwa tuzo ni; Azam Media, ITV na Radio One, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), Jamii Forum, HB TV, Ayo TV na DarMpya TV.

Vingine ni; Wapo Radio, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), East African Televisheni (EATV), Uhuru Publications Limited, The Gurdian Limited, Tanzania Standard Newspapers (TSN), Wasafi Media, Mwananchi, Michuzi Blogsport, Zanzibar Leo, EFM, Clouds Media na Times FM.

error: Content is protected !!