October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Takukuru yaanza kuichunguza Chadema, vigogo wahojiwa

Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imeanza kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, inazokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hivi karibuni, kumekuwepo na madai yanayotolewa na baadhi ya wabunge juu ya matumizi mabaya ya fedha walizochanga kila mwezi kwa mujibu wa Katiba.

Baadhi ya waliotoa shutuma hizo ni; wabunge wa viti maalum; Susan Maselle, Joyce Sokombi na Peter Lijualikali wa Kilombero ambao wote wametangaza kukihama chama hicho.

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao, Maselle na Sokombi walisema mara baada ya Bunge kuvunjwa watahamia NCCR-Mageuzi huku wakisema, hawana shida na kuchangia fedha hizo lakini matumizi yake hayaeleweki.

Leo Jumatano, tarehe 27 Mei 2020, MwanaHALISI ONLINE limemtafuta Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, kujua kama kuna hatua zaidi zimechukuliwa dhidi ya tuhuma hizo ambapo amesema, wameanza kuwahoji baadhi ya watu.

Amesema, wameanza kuwahoji wanachama waandamizi  na viongozi wa Chadema, wabunge waliotoa tuhuma hizo, pamoja na maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, kuna matumizi mabaya ya fedha za michango ya wanachama, ambayo kwa mujibu wa katiba yao wanadai imeanishwa wachangie.”

“Lakini, matumizi yake ndio wanatilia mashaka, kuna fedha nyingi zinatumika ndivyo sivyo, kwa mujibu wa makubaliano yao,” amesema Jenerali Mbungo.

“Kwa hiyo, tunachunguza matumizi yasiyo sahihi ya fedha zao, Takukuru inayomamlaka ya kuchunguza taasisi yoyote iwe ya umma, watu binafsi, chama, klabu, iwe chochote Takukuru wanaingia kufanya uchunguzi, ilimradi kuwe na ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha na rushwa,” amesema bosi huyo wa Takukuru.

Mbungo amewataja baadhi ya watakaohojiwa ni; Dk. Vincent Mashinji, aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, ambaye kwa sasa amehamia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, pamoja na mhasibu mkuu wa chama hicho, Dk. Roderick Lutembeka.

Aidha, Jenerali Mbungo amesema wameshindwa kumhoji Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, kuhusu sakata hilo, kwa kuwa aliieleza TAKUKURU kwamba yuko nje ya jiji la Dar es Salaam.

Amesema, taasisi hiyo imeshaanza kukusanya nyaraka mbalimbali, zinazohusiana na tuhuma hizo.

“Tumeshapata nyaraka kutoka sehemu mbalimbali, wametupatia nyaraka, wamekuwa wanatoa ushirikiano katika hili,” amesema Mbungo.

Jumamosi ya tarehe 23 Mei 2020, Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, alikanusha tuhuma hizo, akisema kwamba, hakuna uthibitisho unaoonesha chama hicho kina matumizi mabaya ya fedha.

Kigaila alisema, fedha za michango ya wabunge na zinazotoka kwa wadau wengine wa Chadema, matumizi yake hupangwa na vikao vyake vya chama, wakati bajeti ya matumizi hayo ikipitishwa na baraza kuu, kisha taarifa zake hutolewa na kamati kuu ya chama hicho.

Kigaila alisema, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hukagua taarifa za matumizi ya Chadema,  na kwamba kwa mujibu wa ukaguzi huo, hakuna ushahidi kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

error: Content is protected !!