November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TAKUKURU: Rushwa ya ngono ipo, fichueni

Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru

Spread the love

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, imewataka wananchi kufichua vitendo vya rushwa ya ngono wanavyokutana navyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa na Brugedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru katika salamu za kilele cha ‘Siku ya Kimataifa ya Wanawake,’ leo tarehe 8 Machi 2021.

Mbungo amesema, rushwa ya ngono ni kitendo cha mtu kutumia madaraka au dhamana aliyopewa kuomba au kulazimisha tendo au upendeleo wa kingono kutoka kwa mtu anayetaka kumhudumia.

Amesema, Februari 2020, Takukuru ilifanya utafiti wa kina katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), lengo likiwa kupata taarifa za kisayansi zitakazosaidia kukabiliana na kero ya rushwa ya ngono kwenye taasisi za elimu ya juu.

Mbungo amesema, matokeo yalionesha “tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyuo tafitiwa lipo; wanafunzi asilimia 58 na watumishi asilimia 60 walieleza kuwepo kwa matukio ya vitendo vya rushwa ya ngono.”

Amesema, utafiti ulibaini sababu za kuwepo kwa tatizo hilo, ni kutokana na mifumo dhaifu ya kudhibiti matumizi mabaya ya mamlaka na mifumo dhaifu ya kusimamia uwajibikaji.

Pia, mfumo dhaifu wa ajira hasa za wahadhiri, kuwa na ufinyu wa huduma muhimu kama hosteli na mikopo ya elimu na kuongezeka kwa wanafunzi pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo amesema, utafiti ulibaini mbinu zinazotumika kushawishi rushwa ya ngono ni kutoa alama za chini kwenye mitihani, vitisho vya kutofaulu kwa wanafunzi, kutoa ahadi kama kumpatia ajira na cheo.

Pia, kumpa chumba chuoni, nafasi ya uongozi, kuongezea utoaji wa huduma na wahadhiri kuwaita wanafunzi kwenye mazingira yasiyo rasmi kwa ajili ya kukagua kazi zao.

Mbungo amesema, kutokana na athari za rushwa ya ngono, Oktoba 2019, kwa kushirikiana na Shirikla lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT), walizindua kampeni iitwayo ‘’Vunja ukimya kata rushwa ya ngono.”

“Niwasihi wananchi kuwafichua wadhalimu wanaodai rushwa ya ngono na rushwa nyingine ili kwa ushirikiano huo, tukomeshe vitendo hivyo,” amesema Mbungo.

error: Content is protected !!